• HABARI MPYA

    Friday, December 15, 2017

    ZANZIBAR HAOOOO FAINALI KOMBE LA CHALLENGE, WAWAVUA UBINGWA UGANDA

    Na mwandishi Wetu, KISUMU 
    ZANZIBAR imefanikiwa kwenda fainali ya kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na CECAFA Challenge baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa watetezi, Uganda jioni ya leo Uwanja wa Moi mjini Kisumu, Kenya.
    Zanzibar sasa itakutana na wenyeji, Kenya kwenye mchezo wa fainali Jumapili Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos, hayo yakiwa marudio ya mchezowa Kundi A uliomalizika kwa sare ya 0-0 Desemba 9.
    Kenya walitangulia fainali jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Burundi kwenye Nusu Fainali ya kwanza iliyodumu kwa dakika 120, baada ya dakika 90 kumalizika timu hizo zikiwa hazijafungana. 
    Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa Twagirumukiza Abdoul Karim, aliyesaidiwa na Theo Ndagijimana wote wa Rwanda na Tigle Belachew wa Ethiopia dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
    Abdulaziz Makame Hassan alianza kuifungia Zanzibar Heroes dakika ya 22 akimalizia kona ya chini chini ya beki, Adeyoum Ahmed Seif ambayo mabeki wa Uganda walizembea kuokoa hadi mchezaji huyo akageuka na mpira na kufunga.
    Baada ya bao hilo, kocha wa Uganda, Moses Basena alifanya mabadiliko akimtoa beki Shafiq Bakari na kumuingiza Joseph Nsubuga dakika ya 26.
    Na dakika mbili baadaye, Uganda wakasawazisha bao hilo kupitia kwa Derrick Nsibambi aliyefunga dakika ya 28 akimalizia krosi ya Allan Kyambadde.
    Kipindi cha pili timu zote zilianza kwa kusukuma mashambulizi na mchezo ukazidi kuchangamka, lakini bahati ilikuwa ni ya Wazanzibar jioni ye leo.
    Mohamed Issa ‘Banka’ alimtungua kipa Ismail Watenga dakika ya 57 kwa mkwaju wa penalti kuipatia Heroes bao la pili baada ya Ibrahim Hamad Ahmada ‘Hilika’ kuangushwa na Nsubuga Joseph ndani ya boksi dakika ya 55.
    Refa Twagirumukiza Abdoul Karim alimtoa kwa kadi nyekundu Nsubuga kwa rafu aliyomchezea Hamad Hilika na Korongo wa Uganda wakaanza kurukaruka kinyonge tangu hapo. 
    Zanzibar wakawa huru mno uwanjani baada ya kadi hiyo, ingawa dakika za mwishoni walilazimika kucheza kwa kujihami na kupoteza muda ili kuulinda ushindi wao.
    Kikosi cha Uganda kilikuwa; Watenga Ismail, Bernard Muwanga, Shafiq Bakari/Joseph Nsubuga dk26, Aggrey Madoi, Nicholas Wadada, Tadfeo Lwanga, Allan Kyambadde/Nelson Senkatuuka dk68, Milton Kalisa, Derrick Nsibambi, Hood Kawesa na Muzamil Mutyaba/Alan Katerega dk59.    
    Zanzibar; Mohammed Abulrahman Mohamed ‘Wawesha’, Ibrahim Mohamed/Ibrahim Abdallah dk87, Adeyum Ahmed, Abdallah Kheri, Issa Haidari, Abdulaziz Makame, Mohamed Issa ‘Banka’, Mudathir Yahya, Ibrahim Hamad ‘Hilika’, Feisal Salum/Mohammed Othman dk64 na Suleiman Kassim ‘Seleembe’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZANZIBAR HAOOOO FAINALI KOMBE LA CHALLENGE, WAWAVUA UBINGWA UGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top