• HABARI MPYA

  Sunday, December 17, 2017

  NGASSA ANGEJUA PANDA SHUKA ZA NDIKUMANA, ASINGEKATA TAMAA

  BILA shaka Suleiman Yamin Ndikumana si jina geni kwenye masikio ya wapenzi wa soka nchini, mchezaji huyo wa kimataifa wa Burundi aliyezaliwa Machi 18, mwaka 1987 kwa sasa anachezea klabu ya Al-Mesaimeer SC ya Qatar.
  Al-Mesaimeer SC iliyokuwa inajulikana kama Al-Nahda SC na baadaye Al-Shoala, yenye maskani yake mjini Mesaimeer inashiriki Ligi Kuu ya Qatar, ijulikanayo kama Qatar Stars League. 
  Kisoka, Ndikumana aliibukia AS Inter Star ya kwao, Bujumbura kabla ya mwaka 2006 kujiunga na vigogo wa Tanzania, Simba SC ambayo Januari mwaka 2008 ilimuuza Molde FK ya Norway.
  Desemba 8, mwaka huo (2008), Ndikumana akasaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu Lierse S.K. ya Ubelgiji wakati huo ikiwa Daraja la Pili.
  Hata hivyo, hakuwa na wakati mzuri Ubelgiji na baada ya kuwekwa benchi mfululizo, akaachwa na kurejea Burundi mwaka 2010 na kujiunga na klabu ndogo tu ya kwao, Fantastique ya Bujumbura.
  Baada ya kazi nzuri katika Ligi ya Burundi, Januari mwaka 2013 Ndikumana akachukuliwa na El-Merreikh SC ya Sudan, ambayo iliamua kumchukua mchezaji huyo baada ya kumkosa Mtanzania, Mrisho Khalfan Ngassa.
  Ndikumana akaanza kupaa tena na Januari 31 mwaka 2014 akajiunga na KF Tirana ya Albania na akawa na wakati mzuri sana na klabu hiyo ya kusini mwa Ulaya, ingawa kwa sababu za kimaslahi Juni mwaka 2015 akaamua kurejea Afrika kujiunga na C.D. Primeiro de Agosto ya Angola.
  Mambo hayakumuendea vizuri Angola akaachwa yeye pamoja na wachezaji wengine watano mwishoni mwa msimu na Januari 29 mwaka 2016 akiwa na nyota mwingine wa Burundi, Fuadi Ndayisenga wakasaini Vital'O FC ya nyumbani kwao, Bujumbura.
  Baada ya kazi yake nzuri tena katika Ligi ya Burundi, Julai 27 mwaka jana (2016), Ndikumana akanunuliwa na Al-Mesaimeer SC na anaendelea vizuri katika Ligi ya Qatar.
  Usemi wa wahenga kwamba ‘Maisha ni kupanda na kushuka’ unadhihirishwa vizuri na historia ya maisha ya kisoka ya Ndikumana na bila shaka ndani ya mafanikio yake kuna uvumilivu na kutokata tamaa.
  Kwa nini leo ninamuelezea Ndikumana? Nitawaambia. Mwisho Khalfan Ngassa ni mwanasoka wa kihistoria katika soka ya Tanzania kwa sasa akiwa anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi za timu ya taifa na pia kufunga mabao mengi.
  Tangu mwaka 2009, hadi mwaka jana alipoitwa mara ya mwisho kwenye kikosi cha Taifa Stars, Ngassa amecheza mechi 100 na kufunga mabao 25.
  Ni juzi tu Ngassa ameachwa na klabu ndogo ya Mbeya City ya nyumbani Tanzania na hata hivyo akafanikiwa kujiunga na klabu nyingine ndogo pia, Ndanda FC ya Mtwara, zote za Ligi Kuu.
  Ngassa ni mchzaji ambaye amecheza klabu zote kubwa Tanzania, Azam, Simba na Yanga kabla ya kwenda Afrika Kusini kujiunga na Free State Stars na baadaye Fanja ya Oman.
  Hakuwa na mafanikio katika klabu zote za nje ya Tanzania – na inakumbukwa amewahi kufanya majaribio West Ham United ya England mwaka 2009 ambako alipelekwa na Yussuf Bakhresa. Alimvutia kocha wa West Ham wakati huo, Gianfranco Zola, lakini akasema kijana hana mwili, arejee  Afrika kujenga mwili.
  Hata hivyo, aliporejea Afrika Ngassa akanogewa na maisha ya soka ya Tanzania na umaarufu wa hapa nyumbani wa kupapatikiwa na wanawake na kupewa ofa nyingi na matajiri wanaopenda kuwa karibu na watu maarufu.
  Pamoja na kubadili jezi za timu zote maarufu nchini Simba, Yanga na Azam – lakini Ngassa pia alipata nafasi ya kwenda kutengeneza tangazo la Utalii nchini Marekani Julai mwaka 2011, ambayo ilimlazimu kuingia uwanjani kuichezea Seattle Sounders FC dhidi ya Manchester United katika mchezo wa kirafiki akiingia kutokea benchi zikiwa zimebaki dakika nane.
  Ngassa alikuwa mwenye kujiamini kutokana na uwezo wake, kipaji cha kuzaliwa ambavyo vyote bado anavyo, isipokuwa tu vinadhoofishwa na msongo wa mawazo unaotokana na kuporomoka kwake kimaisha.
  Watanzania wengi wetu hatutakiani mema na si ajabu wapo wanaofurahia anguko la Ngassa kwa sasa, wakiwemo walionufaika naye wakati akiwa juu.
  Inawezekana kuna sehemu Ngassa alikosea, lakini makosa tumeumbiwa wanadamu hata nasi, tukiwemo mimi na wewe tumewahi kukosea na siku zote hayo makosa ndiyo yanatufundisha.
  Katika kipindi hiki kigumu kwake, Ngassa anahitaji kuwa na moyo sugu na kuelekeza nguvu zake kwenye bidii ya mazoezi ili kuurudisha uwezo wake juu afanye vizuri katika Ligi Kuu akiwa huko huko Ndanda.  
  Naamini ni mchezaji mwenye kipaji na uwezo wa kucheza soka ya ushindani kwa kiwango cha juu kwa zaidi ya miaka mitano ijayo – na anaweza kuinuka tena na kuwasuta wanaombeza kwa sasa.  Ajitahidi kupita njia aliyopita Ndikumana, ambaye alirudi mara kadhaa nyumbani kucheza kwa ujira mdogo kujipanga upya. Kila na heri Ngassa, mbele ya Mungu yote yanawezekana.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA ANGEJUA PANDA SHUKA ZA NDIKUMANA, ASINGEKATA TAMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top