• HABARI MPYA

    Wednesday, October 11, 2017

    MSUVA: TELELA NI KATI YA WACHEZAJI SIWEZI KUWASAHAU MAISHANI MWANGU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happugod Msuva amesema kwamba kiungo Salum Abdul Telela ni kati ya wachezaji waungwana aliokutana nao Yanga SC na hawezi kuwasahau kwa wema wao daima.
    Msuva alikwenda kumtembelea Telela mwishoni mwa wiki kabla ya kurejea Morocco kufuatia kuja nchini kuichezea timu ya taifa mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi Jumamosi.
    Na mfungaji huyo wa bao la kusawazisha la Tanzania katika sare ya 1-1 Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam akaenda kumtembelea mchezaji mwenzake wa zamani wa Yanga baada ya mchezo huo.
    Simon Msuva (kuli) akiwa na Salum Telela baada ya kumtembelea mwishoni mwa wiki
    “Nilikwenda kumtembelea Telala, kwa sababu ni rafiki yangu sana na tumetoka mbali, tuna historia, alinipokea vizuri Yanga na akaishi na mimi vizuri sana. Hata alipoondoka niliumia sana,”alisema Msuva akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana kwa simu kutoka Morocco.
    Msuva amesema kwamba Telela ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa sana na ambaye anaweza kucheza timu yoyote nchi yoyote. “Mwenyewe ameamua kurudi masomoni,  mambo ya soka hayapi kipaumbele tena,”amesema ambaye pia alitembelea timu yake ya zamani, Yanga mazoezini.
    Winga Simon Msuva akiwa mazoezini na klabu yake, Difaa Hassan El Jadida jana nchini Morocco 
    Msuva tayari yupo Morocco na klabu yake, Difaa Hassan El Jadida inatarajiwa kuwa na mchezo wa Kombe la Ligi nchini humo usiku wa leo.
    Kiwango cha Msuva kinaonekana kupanda kwa kasi tangu amehamia Morocco na hilo linadhihirishwa na mchango wake katika timu ya taifa, baada ya kufunga mabao yote katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana mwezi uliopita na Jumamosi akafunga moja katika sare ya 1-1 na Malawi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA: TELELA NI KATI YA WACHEZAJI SIWEZI KUWASAHAU MAISHANI MWANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top