• HABARI MPYA

  Sunday, October 22, 2017

  LWANDAMINA KUWAPUMZISHA YONDAN, JUMA ABDUL NA RAPHAEL LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mzambia wa Yanga, George Lwandamina amesema kwamba anaweza kuwapumzisha wachezaji wake watatu wenye kadi za njano mbili kila mmoja katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo dhidi ya wenyeji, Stand United Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu leo asubuhi, Lwandamina amesema anaweza kuwapumzisha mabeki Juma Abdul, Kevin Yondan na kiungo Raphael Daudi ili kuwaepusha na kuongezewa kadi kabla ya mechi dhidi ya mahasimu, Simba SC Jumamosi ya wiki ijayo.
  Yanga inataremka Uwanja wa Kambarage leo kuwakabili wenyeji, Stand United wakihitaji ushindi ili kuwafikia mahasimu wao Simba SC, wenye pointi 15 baada ya mechi saba za Ligi Kuu.
  Kevin Yondan akimdhibiti mshambuliaji wa Simba, Laudit Mavugo

  Kama Yanga itashinda leo, maana yake mchezo wa mahasimu wa jadi katika soka ya Tanzania utakuwa na ladha mara mbili Oktoba 28, kwani mshindi ndiye atakayetanua kwapa zake kileleni.
  Katika mechi za Ligi Kuu jana, Mtibwa Sugar ilifikisha pointi 15 sawa na Simba SC baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Manungu, Turiani, mkoani Morogoro, bao pekee la beki Dickson Daudi dakika ya 83 akimalizia pasi ya mkongwe mwenzake, mshambuliaji Hussein Javu.
  Simba SC ilishinda 4-0 dhidi ya Njombe Mji FC Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, kiungo Muzamil Yassin akifunga mabao mawili, Mganda Emmanuel Okwi moja sawa na Mrundi, Laudit Mavugo.
  Azam FC ilitoa sare ya pili mfululizo Kanda ya Ziwa, baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, wakitoka kutoa sare ya 1-1 na Mwadui FC wiki iliyopita Shinyanga.
  Mbeya City nayo iliichapa mabao 2-0 Ruvu Shooting Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wafungaji Elius Ambokile dakika ya 36 na Frank Hamisi Ikobelo dakika ya 52, wakati Lipuli iliilaza 1-0 Maji Maji ya Songea Uwanja wa Samora mjini Iringa, mfungaji Moka Shaaban na Ndanda FC imelazimishwa sare ya 0-0 Singida United Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LWANDAMINA KUWAPUMZISHA YONDAN, JUMA ABDUL NA RAPHAEL LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top