• HABARI MPYA

    Sunday, October 22, 2017

    HATUWEZI KUUTOKOMEZA USHIRIKINA MICHEZONI, KAMA VIONGOZI WETU WENYEWE NI WASHIRIKINA

    MWEZI huu utabaki kuwa wa kihistoria Tanzania, kwani ndio ambao taifa lilimpoteza mwasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999 katika hospitali ya Mtakatifu Thomas Jijini London, Uingereza alipokuwa amelazwa kwa matibabu ya saratani ya damu.
    Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa mengi marehemu Mwalimu Nyerere, kubwa ni kujenga taifa lenye umoja, mshikamano, amani na upendo kwa kuhakikisha kwa namna yoyote wananchi wake hawayumbishwi na udini wala ukabila.
    Watanzania wanajua namna sumu ya ukabila ilivyozitafuna baadhi ya nchi, wakiwemo majirani zetu Rwanda na Burundi – hakika ni mambo ya kusikitisha mno.
    Katika kupiga vita ukabila, Mwalimu Nyerere alikuwa mkali mno na akawaambia wananchi wake kwamba dhambi ya ubaguzi wa kikabila ni mbaya na tukithubutu kuijaribu hatutaacha na huo utakuwa mwanzo wa taifa letu kuangamia.
    Alipiga sana vita ukabila wakati wa chokochoko za kutaka kuuvunja Muungano, akisema leo tukitaka kutengana kwa Uzanzibari na Utanganyika, kitakachofuata ni kutengana kwa ukabila, mfano Upemba na Uzanzibari.
    Hakuishia hapo Mwalimu, alipiga vita na udini. Alikuwa akisema Tanzania haina dini, bali wananchi wake ndio wana dini na aliruhusu uhuru wa kuabudu, lakini hakuna mtu aliyeshurtishwa siyo tu kuwa wa dini fulani, bali hata kuwa na dini.
    Na mwalimu alikuwa akimtolea mfano mmoja wa rafiki zake na viongozi wenzake enzi za utawala wake, Kingunge Ngomale Mwiru ambaye alikuwa hana dini, lakini aliendelea kuheshimiwa na kuthaminiwa.
    Wakati tukiwa katika mwezi wa kumbukumbu ya kifo cha baba wa taifa letu, Mwalimu Nyerere, tunapaswa kuchukua mifano mingi mizuri ya harakati zake tofauti katika kuendeleza ustawi wa Tanzania nzuri yenye kumpendeza yeyote katika nyanja zote.
    Katika michezo pia kuna vita nyingi na kubwa – zaidi ni kudumaa kwa michezo yenyewe, hali inayolifanya taifa letu siku zite liburuze mkia kwenye mashindano mbalimbali.
    Tukiitisha kongamano la kupokea maoni ya kwa nini michezo imezorota nchini sababu nyingi zitatajwa kuanzia kutowekeza kwenye michezo ya watoto na vijana, yaani kuwa na akademi za wanamichezo wachanga, kukosekana wataalamu, vifaa vya michezo, maeneo ya kuchezea, sera mbovu na hata Serikali yenyewe kutotenga bajeti ya kusaidia michezo.
    Matatizo hayo yakiwepo, bado nchi imeendeleea kujikongoja na kushiriki michezo, lakini kuna matatizo mengine yanaibuka na kutukwamisha pia, ikiwemo kuabudu imani za kishirikina.
    Mara kadhaa Bodi za michezo nchini, likiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa adhabu kwa wanamichezo na timu kwa sababu ya kuwahusisha na imani za kishirikina.
    Lakini ukizama ndani, unakuta viongozi hao hao wa TFF wanaidhinisha mambo ya kishirikina kufanyika kwenye timu za taifa na wachezaji wanajua kwamba shirikisho lao la soka limewaletea mganga awalogee washinde.
    Mchezaji ambaye ameshiriki mambo ya kishirikina katika timu ya taifa, atawezaje kusita kuyafanya katika klabu au yeye mwenyewe kibinafsi? Wakati mwingine tunawaharibu hadi wanasoka wetu chipukizi kwa kuwaaminisha ushirikina mapema.
    Mchezaji anaumia uwanjani, badala ya kufuata tiba za kitaalamu anaamini amelogwa na kwenda kwa waganga, ambako kwanza analiwa fedha zake bure na haponi matokeo yake tumepoteza wachezaji wengi nyota mapema.
    Tutafanikiwa kuutokomeza ushirikina michezoni, iwapo viongozi wetu watasimama kidete na kuupinga kwa dhati na kupambana nao wazi, kwanza kuhakikisha mambo hayo hayafanyiki tena kwenye timu za taifa.
    Hatuwezi kufanikiwa kuutokomeza ushirikina, kama viongozi wetu wenyewe ni washirikina, zaidi tutaishia kujikosha kwa kuzitoza faini klabu na wanamichezo tu kwa vitendo vya kishirikina.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATUWEZI KUUTOKOMEZA USHIRIKINA MICHEZONI, KAMA VIONGOZI WETU WENYEWE NI WASHIRIKINA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top