• HABARI MPYA

    Monday, October 02, 2017

    ETOILE YAICHAPA 2-1 AL AHLY, MAZEMBE YASHINDA 1-0

    MABAO ya kila kipindi ya Alaya Brigui na Mohamed Ben Amor yameipa Etoile Sportive du Sahel ushindi wa 2-1 dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika jana Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse.
    Wenyeji waliuanza mchezo vizuri na kufanikiwa kupata bao la kuongoza lililofungwa na Alaya Brigui dakika ya 16 na Etoile Sahel waliendelea kutawala mchezo baada ya bao hilo, lakini wakawa wabovu kwenye umaliziaji.
    Vigogo wa Misri wakarudi na nguvu mpya kipindi cha pili na kuanza kupeleka mashambulizi langoni mwa wenyeji wao na katika dakika ya 65, Salah Gomaa akaisawazishia Ahly.
    Hata hivyo, furaha ya Wamisri haikudumu sana, kwani Etoile Sahel ilifanikiwa kufunga bao la pili dakika 10 baadaye, mfungaji Mohamed Ben Amor.
    Etoile du Sahel wameshinda 2-1 jana dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa 

    Pamoja na Al Ahly kujaribu kurudisha bao hilo, lakini Etoile Sahel walisimama imara na kuulinda ushindi wao mwembamba wa ugenini.
    Timu hizo sasa zitarudiana wiki tatu zijazo katika mchezo wa kuamua timu ya kwenda fainali, ambako watakutana na mshindi kati ya USM Alger na Wydad Casablanca zilizotoka suluhu (0-0) katika mchezo wa kwanza nchini Morocco Ijumaa usiku.
    Kikosi cha Etoile Sahel kilikuwa: Mathlouthi, Nagguez, Konate, Boughattas, Abderrazzak, Brigui, Ben Amor, Msakni, Trabelsi, Bangoura, Marei/Chermiti dk79.
    Al Ahly: Ekramy, Fathy, Rabia, Samir, Maaloul, Soleya, Hesham Mohamed/Hany dk46, El-Said, Soliman, Azarou/Gomaa dk65 na Ajayi.
    Wakati huo huo: TP Mazembe jana ilipata ushindi mwembamba wa 1-0 nyumbani dhidi ya FUS Rabat ya Morocco katika Nusu Fainali ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho, bao pekee la Ben Malango Ngita dakika ya 14 Uwanja wa TP Mazembe, Lubumbashi.
    Bao la Thabo Mnyamane dakika ya 87, jana liliwanusuru SuperSport United kulala nyumbani mbele ya Club Africain ya Tunisia Uwanja wa Lucas Moripe mjini Johannesburg, Afrika Kusini baada ya kupata sare ya 1-1 kufuatia Saber Khalifa kuwafungia wageni bao la kuongoza kwa penalti dakika ya 21 katika Nusu Fainali nyingine ya Kombe la Shirikisho.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ETOILE YAICHAPA 2-1 AL AHLY, MAZEMBE YASHINDA 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top