• HABARI MPYA

    Wednesday, October 04, 2017

    DOMAYO: MAFANIKIO YA AZAM NI UMOJA NA KUCHEZA KAMA TIMU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa Azam FC, Frank Domayo ‘Chumvi’, amesema kwamba moja ya vitu vinavyowabeba hadi kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ni kucheza pamoja kama timu na kushikamana.
    Azam FC imekuwa na mwanzo mzuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na baada ya mechi tano, mabingwa hao wa zamani wamejikusanyia jumla ya pointi 11 sawa na Mtibwa Sugar na Simba zilizo juu yake kwa tofauti ya mabao.
    “Siri ya mafanikio ni kujituma, kufanya mazoezi kuishi na watu pamoja wachezaji wenzangu tunaoshirikiana uwanjani, kupendana, mkipendana siku zote mnasaidiana kwa kila jambo kama mtu umekosea tunakupa moyo, sehemu mtu ya kufunga unamwekea mwenzako, kwa hiyo naweza kusema tunacheza kwa pamoja ili tuweze kufanya vizuri,” alisema.
    Frank Domayo akimpita Seif Abdallah Karihe wa Lipuli katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wiki mbili zilizopita 

    Kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha timu mbele na kusaidia ukabaji, amesema kuwa wanapambana ili waweze kushinda kila mechi wanayoingia dimbani ili timu hiyo iwe na mwisho mzuri.
    “Kwa hiyo tunapambana kadiri ya uwezo wetu kila mechi inayokuja ili tuweze kufanya vizuri na tuweze kushinda, kila timu ina changamoto, kwa hiyo kama hamna changamoto kunakuwa hamna kitu kwenye timu, naweza kusema kuwa tunapambana kila mtu kwenye nafasi yake, unapigania namba yako ili uweze kucheza vizuri kila mechi ili uweze kudumu kwenye kikosi.
    “Kuna wachezaji wengi wazuri kocha mwenyewe anachagua kwa hiyo unapambana kwenye nafasi yako, unafuata maelekezo ya kocha na unacheza kulingana na kocha anachokuagiza uwanjani ili uweze kumshawishi aweze kukupa nafasi,” alisema.
    Baada ya mapumziko ya siku mbili jana na leo Jumanne, kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa nchini ya NMB na Tradegents, kinatarajia kurejea tena mazoezini kesho Jumatano jioni kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mwadui unaotarajia kufanyika Uwanja wa Mwadui Complex Oktoba 14 mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DOMAYO: MAFANIKIO YA AZAM NI UMOJA NA KUCHEZA KAMA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top