• HABARI MPYA

    Saturday, August 05, 2017

    SIMBA MAKAO MAKUU WAWAFARIJI YATIMA MAGOMENI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KITUO cha kulea watoto yatima cha Umra Ophanage kilichoko Magomeni jijini Dar es Salaam leo kimepokea msaada wa chakula mbalimbali kutoka kwa Kundi la Wanachama wa Simba liitwalo Simba HQ.
    Msaada huo wa chakula ambao umejumuisha mchele, sembe, sukari, ngano, sabuni, mafuta ya kula, maharage, chumvi na maji una thamani ya Sh. milioni 2.2/.
    Akizungumza kwa niaba ya kundi hilo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kupunguza makali kwa walezi ambao wanaishi na watoto hao kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara akikabidhi misaada hiyo leo

    Manara alisema kuwa anafahamu msaada huo hautamaliza changamoto ambazo zinawakabili lakini anaamini kwa siku chache kitawasaidia watoto hao waweze kuishi katika mazingira mazuri kama watoto wengine ambao wanaishi na wazazi wao.
    "Hatutoi kwa sababu tunataka jamii ijue, lakini lengo letu ni kuhamasisha na watu wengine waje kutoa, waje kusaidia watu, wajitokeze kusaidia, hatuwezi kusikia furaha kama tunachokipata hatujirejeshi kwa jamii kama hii inayohitaji msaada," alisema Manara.
    Naye Mkurugenzi wa kituo hicho, Rahma Kishumba, aliwashukuru wanachama hao wa Simba kwa msaada ambao wamewapatia na kueleza kuwa hii si mara ya kwanza kwa klabu hiyo kuwatembelea.
    Mkurugenzi huyo aliitakia Simba mafanikio katika msimu mpya wa ligi huku pia akiwataka taasisi na makampuni mengine kujitokeza kuwasaidia hasa katika changamoto ya vifaa vya elimu kwa sababu analea watoto wa kuanzia chekechea hadi chuo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA MAKAO MAKUU WAWAFARIJI YATIMA MAGOMENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top