• HABARI MPYA

    Monday, August 07, 2017

    MGOMBEA TFF AJA NA MIPANGO ‘BABU KUBWA’, NI MULAMU NGHAMBI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MGOMBEA nafasi ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mulamu Erick Nghambi  ameahidi kuendeleza mpira wa miguu kwa kushirikiana na mikoa yote kwa kutumia mpango mkakati wa kitaifa, ambao ndio utakuwa ndio dira ya mchezo huo nchini endapo atachaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma.
    Akizungumza kwenye mkumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam leo kwenye uzinduzi wa kampeni zake, Nghambi amesema endapo atapata nafasi hiyo ataitendea haki kutokana na uzoefu alionao baada ya kutumikia nyadhifa mbalimbali katika soka hapa nchini.
    Mulamu Ng'ambi  ameahidi kuendeleza soka nchini akichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TFF katika uchaguzi wa Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma

    Nghambi amesema dira yake imegawanyika katika maeneo matatu, ambayo ni mipango muda mfupi, wa kati na muda mrefu – ambayo italeta mapinduzi makubwa katika soka ya Tanzania.
    Kuhusu mipango ya muda mfupi, amesema kwamba atasimamia udhibiti wa fedha kwenye  shirikisho kwa kuziba mianya yote ya upotevu au matumizi ambayo hayana ulazima pamoja na kuongeza mapato kwa kutumia njia ya mawasiliano kwa kutumia njia maalum watakazotengeneza.
    Kuhusu mipango ya muda wa kati, Nghambi amesema atashirikiana na Kamati ya Utendaji katika kuboresha Ligi, kuanzia Ligi Kuu hadi Ligi ya Mabingwa wa Mkoa kwa  kuongeza udhamini  kwenye ligi hizo.
    Na kwenye mipango ya muda mrefu, Nghambi amesema atafanya marekebisho makubwa katika hosteli za TFF zilizopo makao makuu ya shirikisho hilo, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam ziwe katika kiwango cha nyota tatu, ili ziweze kutumika kwa timu za taifa pale zitakapohitajika kuingia kambini.
    “Hii itasaidia kupunguza gharama kubwa ambazo zimekuwa zikitumika kulipa kambi katika hoteli mbalimbali, ili kuhakikisha mpira unapiga hatua kwa kushirikiana na mashirikisho mengine duniani kwa kuandaa semina mbalimbali kwa ajili ya viongozi wa klabu,”amesema Nghambi.
    Katika nafasi hiyo, Nghambi anachuana na Michael Wambura, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa wakati wagombea Urais ni Ally Mayay, Frederick Mwakalebela, Imani Madega, Wallace Karia, Shija Richard na Emmanuel Kimbe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MGOMBEA TFF AJA NA MIPANGO ‘BABU KUBWA’, NI MULAMU NGHAMBI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top