• HABARI MPYA

    Thursday, February 19, 2026

    TFF YAZIINGIZA KAMPUNI ZA KUBASHIRI KWENYE ‘VITA’


    SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeziingiza kwenye ushindani mkali kampuni za michezo ya kubashiri baada ya kutangaza rasmi zabuni ya haki ya kubashiri mchezo wa watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba.
    Mchezo huo unaotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi umepangwa kuchezwa Machi Mosi katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, na tayari umeanza kuonekana kama fursa muhimu ya kibiashara kwa sekta ya michezo ya kubashiri.
    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, shirikisho limesema kuwa haki zote za kubashiri michezo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni mali ya TFF pamoja na washirika wake waliotambuliwa kisheria.
    TFF imeeleza wazi kuwa kampuni yoyote ya kubashiri itakayojihusisha na kubashiri mchezo huo au michezo mingine ya ligi bila kuwa mshirika halali wa shirikisho hilo itakuwa imekiuka taratibu na sheria zilizopo.
    Katika taarifa hiyo, shirikisho limetoa onyo kali kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni au taasisi yoyote itakayokaidi maelekezo hayo, ikiwa ni sehemu ya kulinda maslahi ya mpira wa miguu nchini na kuongeza uwajibikaji.
    Baadhi ya wadau wa mpira wa miguu wamesema kuwa hatua hiyo ya TFF inaelezwa kuwa ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika usimamizi wa masuala ya kibiashara kwenye soka la Tanzania, huku ikilenga kudhibiti sekta ya kubashiri, kuongeza mapato halali na kuhakikisha maendeleo endelevu ya mchezo huo.

    Walisema kuwa TFF inatakiwa kuendesha mchakato wa zabuni kwa uwazi na kwa kuzingatia taratibu zote za nchi, huku ikilenga kupata mshirika atakayetoa thamani halisi ya kibiashara kwa mpira wa miguu wa Tanzania.
    Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kupambana na vitendo vya upangaji matokeo kwa kuweka mifumo rasmi ya ufuatiliaji wa miamala ya ubashiri na kushirikiana na mamlaka husika za udhibiti na usalama.
    “Huu ni mwanzo mzuri wa udhibiti wa kupanga matokeo (match fixing) na utasaidia kuongeza mapato yatakayorejeshwa kwenye maendeleo ya soka, ikiwemo uendeshaji wa ligi, uboreshaji wa uamuzi wa waamuzi, maendeleo ya vijana na miundombinu ya michezo,” alisema Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Mwesigwa Celestin.
    Kwa ujumla, wadau wa soka wanaona uamuzi wa TFF kama mwanzo wa zama mpya za usimamizi wa kibiashara katika mpira wa miguu wa Tanzania, ambapo rasilimali za mchezo zinalindwa, thamani yake inaongezeka na manufaa yanarejea moja kwa moja kwenye maendeleo ya mchezo wenyewe.
    Next
    This is the most recent post.
    Older Post
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAZIINGIZA KAMPUNI ZA KUBASHIRI KWENYE ‘VITA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top