• HABARI MPYA

    Saturday, June 17, 2017

    SIMBA YAFIKIRIA KUMTEMA JANVIER BOKUNGU

    Na Shekha Jamal, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC inaweza kuachana na beki Mkongo, Janvier Besala Bokungu baada ya kufanikiwa kumrejesha beki wake wa zamani wa kulia, Shomary Kapombe.
    Bokungu amemaliza mkataba wake Simba SC, lakini uongozi unaona baada ya kumpata Kapombe haina maana ya kuendelea na raia huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa sababu wote wawili ni wachezaji wa hadhi ya kimataifa na wazoefu.
    Na katika kujiandaa na hilo, Simba tayari imemsajili beki chipukizi wa kulia, Ally Shomary kutoka Mtibwa Sugar ili awe mbadala wa Kapombe anapopata dharula.
    Simba inaweza kumtema beki Mkongo, Janvier Besala Bokungu (mwenye mpira) baada ya kumrejesha Shomary Kapombe

    Shomary amesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro ambako kwa misimu miwili iliyopita alikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza.
    Simba wanaamini Kapombe na Ally Shomary watatosha sana kwa beki ya kulia, hivyo Bokungu, beki wa zamani wa TP Mazembe ya kwao na Esperance ya Tunisia, ambaye amemaliza mkataba wake anaweza kuruhusiwa kuondoka, ingawa mazungumzo ya mkataba mpya yalikwishaanza. 
    Simba ipo katika harakati za kuboresha kikosi chake baada ya kufanikiwa kurejea kwenye michuano ya Afrika kufuatia kuikosa kwa miaka mitano.
    Na tayari Simba imekwishasajili wachezaji sita wapya, ambao mbali na Kapombe na Shomary wengine ni kipa Emanuel Elias Mseja, mabeki Jamal Mwambeleko waliosajiliwa kutoka Mbao FC, Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans zote za Mwanza na mshambuliaji John Bocco kutoka Azam FC. 
    Pamoja na hayo, tayari kuna taarifa Simba SC imemsajili kipa namba moja Tanzania, Aishi Manula, huku pia ikiwa mbioni kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani, Mganda Emmanuel Okwi kutoka SC Villa ya kwao.
    Simba inafanya usajili wa kishindo, baada ya kufanikiwa kukata tiketi ya kurejea kwenye michuano ya Afrika mwakani kwa mara ya kwanza baada ya mitano.
    Wekundu hao wa Msimbazi watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, kufuatia kutwaa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Mei 27 mwaka huu kwa kuifunga Mbao FC 2-1 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAFIKIRIA KUMTEMA JANVIER BOKUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top