• HABARI MPYA

  Friday, June 16, 2017

  MBARAKA YUSSUF ATAKA KUITUMIA AZAM KUTIMIZA NDOTO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbaraka Yussuf Abeid amesema kwamba kusajiliwa Azam FC hakumaanishi amemaliza, bali anakabiliwa na changamoto ya kuongeza juhudi ili kukuza kiwango chake aweze kutimiza ndoto zake za kufika mbali zaidi kisoka.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana, Mbaraka amesema kwamba anatakiwa kuongeza juhudi akuze kiwango chake kwanza ili aweze kumudu ushindani wa namba ndani ya kikosi cha Azam na pia kulinda nafasi yake timu ya taifa, Taifa Stars.
  “Hapa nilipofika ndiyo kama ninaanza sasa kukutana na changamoto za kweli za soka, hii timu ya Azam ni kubwa, ina wachezaji wakubwa na wenye uwezo mkubwa, wakiwemo wa kigeni wale Waghana, wale wazuri sana. Inabidi niwe fiti nigombee nao namba,”amesema.
  Mbaraka Yussuf (katikati) amesema anakabiliwa na changamoto ya kuongeza juhudi baada ya kusaini Azam ili kukuza kiwango chake 

  Pamoja na hayo, Mbaraka amesema anapaswa pia kuwa fiti zaidi ili aendelee kuitwa timu ya taifa na ifike wakati awe mchezaji wa kikosi cha kwanza, ili siku moja atomize ndoto zake za kufika mbali zaidi kisoka.   
  Mchezaji huyo aliyeibukia timu ya vijana ya Simba, alishika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akifunga mara 12 na kuzidiwa bao moja na wote, Simon Msuva wa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting waliofungana na kubeba pamoja kiatu cha dhahabu.
  Lakini katika sherehe za kuhitimisha msimu wa VPL, Mbaraka akatunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu akiwaangusha Shaaban Iddi wa Azam FC na Mohammed Issa ‘Banka’ wa Mtibwa Sugar.   
  Mfungaji huyo wa bao la ushindi la Taifa Stars, ikiilaza 2-1 Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Machi 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, alizaliwa Septemba 2 mwaka 1997, Kinondoni, Dar es Salaam na akasoma Shule ya Msingi Kumbukumbu na baadaye sekondari ya Tabata kabla ya kuhamia Kinondoni Muslim alikohitimu Kidato cha Nne.
  Kinondoni Muslim ndiko haswa alikoanzia kucheza soka hadi mwaka 2014 alipokwenda kujiunga na timu ya vijana ya Simba SC ambako alicheza hadi 2015 akapandishwa timu ya kwanza chini ya kocha Muingereza, Dylan Kerr lakini wakati Ligi Kuu inakaribia kuanza akatolewa kwa mkopo Kagera Sugar. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBARAKA YUSSUF ATAKA KUITUMIA AZAM KUTIMIZA NDOTO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top