• HABARI MPYA

  Sunday, June 18, 2017

  KWA USAJILI HUU, TIMU IKIVURUNDA ATAFUKUZWA KOCHA?

  TIMU ya Manchester United inataka kumsajili winga wa Inter Milan, Ivan Perisic kwa dau la Pauni Milioni 44 wiki za karibuni. 
  Jose Mourinho anaona winga huyo wa Inter Milan mwenye umri wa miaka 28 ni miongoni mwa wachezaji muhimu wa kusajili katika mkakati wa kuimarisha kikosi chake angalau kwa kuongeza nyota wapya wanne.
  Hakuna ada iliyokubaliwa, lakini makubaliano ya kimikataba yamefikiwa baina ya klabu hizo na Bin Zubeiry Sports - Online inafahamu kwamba Mreno huyo anamtaka Perisic katika kikosi chake haraka kwa ajili ya ziara ya Marekani mwezi ujao.
  Tayari Mourinho amemsajili beki wa Benfica, Victor Lindelof kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 30.7, dili ambalo lilikamilika Jumatano.
  Pia anataka kumuongeza mshaambuliaji wa Real Madrid, Alvaro Morata achukue nafasi ya Zlatan Ibrahimovic, lakini kuna wasiwasi Old Trafford kwamba mpango wowote wa kumsajili mshambuliaji huyo utaifanya klabu ya Hispania nayo iombe kumsajili kipa wao, David de Gea, mchezaji ambaye hawataki kumpoteza.
  Kiwango cha kipa wao wa sasa, Keylor Navas kimeibua taarifa kwamba Real Madrid imeachana na mpango wa kumfuatilia De Gea, aliyekaribia kujiunga na timu hiyo ya La Liga mwaka 2015 kabla ya kukwama dakika ya mwisho.
  Mwanzo hadi mwisho wa habari hii, ambayo chanzo chek ni Daily Mail Online anatajwa kocha, Jose Mourinho kwamba ndiye anayesajili.
  Habari hii inatoka wakati huu, ambao hata huku kwetu timu zipo katika zoezi la usajili kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Ni timu tano za Ligi Kuu, kati ya zote 16 ambazo hadi sasa zimetangaza kusajili wachezaji wapya, zikiwemo zilizomaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu uliopita, Yanga waliokuwa mabingwa, Simba washindi wa pili, Kagera Sugar washindi wa tatu na Azam FC walioshika nafasi ya nne na Singida United iliyopanda.
  Yanga imewasajili wachezaji wawili tu hadi sasa, beki Abdallah Hajji Shaibu kutoka Taifa Jang’ombe ya Zanzibar na kiungo Pius Busitwa kutoka Mbao FC ya Mwanza, ingawa habari zisizo rasmi zinasema hata kipa Mcameroon.
  Wengine wanaotajwa kuwa kwenye mpango wa kusailiwa Yanga ni Babu Ally Seif kutoka Kagera Sugar, Ibrahim Hajib kutoka Simba na Himid Mao kutoka Azam FC.  
  Simba imewasajili kipa Emanuel Elias Mseja, mabeki Ally Shomary kutoka Mtibwa Sugar, Shomary Kapombe kutoka Azam FC, Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC, Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans na mshambuliaji John Bocco kutoka Azam FC. 
  Pamoja na hayo, tayari kuna taarifa Simba SC imemsajili kipa namba moja Tanzania, Aishi Manula, huku pia ikiwa mbioni kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani, Mganda Emmanuel Okwi kutoka SC Villa ya kwao.
  Kagera Sugar imewasajili wachezaji sita wapya, ambao ni pamoja na beki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba, Juma Said Nyosso, kipa Hussein Kipao kutoka JKT Ruvu iliyoshuka Daraja kutoka Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, beki Japhary Kibaya kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, viungo Peter Samson Mwalyanzi, Ludovic Venance na mshambuliaji Omary Daga maarufu ‘Dagashenko’ wote kutoka Africa Lyon iliyoshuka Daraja pia.
  Azam FC nayo imewasajili kipa Benedict Haule, kiungo Salmin Hoza kutoka Mbao FC ya Mwanza na washambuliaji Waziri Junior kutoka Toto Africans na Mbaraka Yussuf kutoka Kagera Sugar.
  Na kila timu wakati inatangaza mchezaji mpya, viongozi wake wamekuwa wakiusifu usajili huo umefanywa kwa kuzingatia ushauri wa benchi la Ufundi.
  Lakini ukiutazama aina ya usajili unaofanywa hauoni kama unafanana na makocha na ushauri wa wataalamu na waliobobea kama wale wa Yanga, Azam na Simba.
  Unaonekana kabisa ni usajili wa utashi watu na sasa wamekuja na ‘ngonjera’ mpya, eti wanadai kwamba benchi la Ufundi halielekezi mchezaji rasmi wa kusajiliwa bali linapendekeza mchezaji kwa nafasi yake.
  Yaani kwa mfano, benchi linaacha maelekezo asajiliwe beki labda wa kulia, kiungo mchezeshaji na mshambuliaji – labda.
  Kwa hiyo Kamati za Usajili ndizo zinakwenda sasa kusajili hawa wachezaji tunaoona wanasajiliwa kwa sasa.
  Hata tukikubali benchi la Ufundi limependekeza labda kwa mfano pale Simba asajiliwe kipa, beki wa kulia, beki wa kushoto, beki wa kati na mshambuliaji kama walivyosajili, bado kuna maswali.
  Simba imemaliza msimu na makipa watatu, Mghana Daniel Agyei ambaye inasemekana atatemwa, Peter Manyika na Dennis Richard.
  Lakini tayari imesajili makipa wapya wawili, Aishi Manula na Mseja – ambao hata akitemwa Agyei watabaki makipa wanne.
  Lakini huyu kipa wa Mbao alikuwa hachezi kule, kwa sababu kipa wa kwanza alikuwa Erick Ngwengwe ambaye aliondolewa mwishoni mwa msimu akaanza kudaka Benedict Haule aliyechukuliwa Azam.
  Ndiyo, kocha Mcameron Joseph Marius Omog kaagiza asajiliwe makipa wawili na uongozi umefanya hivyo kwa kuwasajili Manula na Mseja. Sasa Rais wa Simba atusaidie tu, alimuona wapi Mseja akavutiwa naye hadi kumsajili wakati Mbao alikuwa hachezi?
  Kweli aina ya usajili huu, halafu baada ya mzunguko wa kwana wa Ligi Kuu timu isipopata matokeo mazuri yanayotarajiwa, atafukuzwa kocha? 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KWA USAJILI HUU, TIMU IKIVURUNDA ATAFUKUZWA KOCHA? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top