• HABARI MPYA

  Tuesday, April 11, 2017

  YANGA WATINGA TAKUKURU KUZUIA POINTI TATU ZA CHEE SIMBA, WADAI KAMATI YA SAA 72 "MANAZI WA MSIMBAZI"

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imesema imeanza mawasiliano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambaa na Rushwa (TAKUKURU) ili waichunguze Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania au Kamati ya Saa 72 kwa madai wanataka kucheza mchezo mchafu kwa kushirikiana na klabu ya Simba.
  Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam kwamba Kamati hiyo kwa kushirikiana na klabu ya Simba wanataka kufoji taarifa za michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ili kuibeba klabu hiyo.  
  Mkemi alisema baada ya Simba kufungwa 2-1 na Kagera Sugar Aprili 2, mwaka huu na kupoteza mwelekeo kwenye mbio za ubingwa wamehamishia nguvu zao nje ya Uwanja kuhakikisha wanatwaa ubingwa.
  Salum Mkemi (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam

  Amesema Simba wanadai beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi alicheza mechi dhidi ya Kagera Sugar akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, wakati alikuwa ana kadi mbili tu.
  “Hiyo kadi nyingine wanayotaka kuchomekea, alioonyeshwa kwenye mechi ya Kombe la TFF. Siyo Ligi Kuu,”alisema.
  Kwa sababu hiyo, Mkemi amesema kwamba wameanza kuwasiliana na TAKUKURU ili waingilia kati suala hilo kwa kuwachunguza Kamti ya Saa 72.
  Amesema pia wamewasiliana na Kitengo cha kukabiliana na uhalifu wa mitandaoni na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kuchunguza taarifa za michezo za waamuzi na makamisaa kuhusu kadi za njano za Fakhi ili kujua zilitumwa lini.
  Kwa ujumla Mkemi amesema kwamba wanataka vyombo vya dola vilifanyie kazi suala hilo kikamilifu ili mbivu na mbichi zijulikane.
  Pamoja na hayo, Mkemi ameishutumu Kamati ya Saa 72 kwamba inaundwa na wajumbe wengi ambao ni wapenzi wa mahasimu wao, Simba na maamuzi yao yanaegemea katika ushabiki.
  Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha beki Mohammed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya uamuzi. 
  Mkemi pia akawapongeza Simba kwa ushindi wa jana wa 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mijini Mwanza ingawa aliubeza ulitokana na ‘kulegea’ kwa wapinzami wao dakika za mwishoni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WATINGA TAKUKURU KUZUIA POINTI TATU ZA CHEE SIMBA, WADAI KAMATI YA SAA 72 "MANAZI WA MSIMBAZI" Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top