• HABARI MPYA

    Monday, April 10, 2017

    SIMBA SC KUREJEA KILELENI LEO?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC inaweza kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo, iwapo itawafunga wenyeji, Mbao FC katika mchezo utaaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Wekundu hao wa Msimbazi wanaingia katika mchezo wa leo, wakitokea Geita walipoweka kambi ya wiki moja wakitokea Bukoba, ambako Jumapili iliyopita walifungwa 2-1 na wenyeji Kagera Sugar na kuangukia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi.
    Mabingwa watetezi, Yanga SC ambao Jumamosi iliyopita waliifunga 1-0 Azam FC ndiyo waongoza Ligi Kuu kwa sasa kwa pointi zao 56 baada ya kucheza mechi 25 wakiwazidi pointi moja tu Simba ambao leo wanacheza mechi ya 26.
    Mshambuliaji tegemeo wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo ataiongoza timu yake leo dhidi ya Mbao FC

    Katika mchezo wa leo, Simba itamkosa beki wake wa kati, Abdi Banda ambaye amesimamishwa kwa muda usiojulikana kucheza Ligi Kuu kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla katika mchezo wa ligi hiyo baina ya timu hizo Aprili 2, Uwanja wa Kaitaba Bukoba.
    Maamuzi hayo hayo yaliyofikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania au Kamati ya Saa 72 Ijumaa mjini Dar es Salaam ni chungu kwa Simba, kwani tayari inamkosa beki wake wa kati tegemeo, Mzimbabwe Method Mwanjali, ambaye ni majeruhi.
    Maana yake, kwa vyovyote leo kocha Mcameroon, Jopseh Marius Omog atalazimika kuwapanga Novaty Lufunga na Juuko Murshid na kwenye benchi hatakuwa na mchezaji wa akiba wa katikati. 
    Simba SC itamkosa pia Nahodha wake, Jonas Mkude kwa sababu ya kadi za njano wakati habari njema tu ni kwamba, beki wa kulia, Mkongo Janier Besala Bokungu anarejea baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mchezo dhidi ya mahasimu, Yanga Februari 25. 
    Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo ni kati ya wenyeji, Mtibwa Sugar na Azam FC Uwanja wa Manungu Turiani, Morogoro. 
    Mechi za juzi Kagera Sugar ililazimishwa sare ya 0-0 na JKT Ruvu Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Ndanda FC ilishinda 2-1 ugenini Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya dhidi ya wenyeji Mbeya City na Maji Maji ililazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon mjini Songea mkoani Ruvuma, wakati jana Stand United iliichapa 1-0 Tanzania Prisons Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUREJEA KILELENI LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top