• HABARI MPYA

    Sunday, April 09, 2017

    POINTI TATU ZA CHEE SIMBA DHIDI YA KAGERA ZAWEKWA KIPORO, YANGA WAPEWA ONYO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imeahirisha kusikiliza malalamiko ya klabu ya Simba dhidi ya Kagera Sugar kumchezesha beki Mohammed Fakhi Gharib akiwa anatumikia adhabu ya kukosa mechi kwa sababu ya kadi za njano hadi Alhamisi.
    Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Simba imemkatia rufaa Mohammed Fakhi (kushoto) kwamba alicheza akiwa ana kadi tatu za njano

    Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya uamuzi.
    Kwa upande mwingine, Yanga imepewa onyo kwa kutoingia kwenye chumba chake cha kubadilishia nguo kwenye mechi namba 195 wakishinda 1-0 dhidi ya Azam. 
    Yanga haikuingia kwenye chumba chake cha kubadilishia nguo, kutokana na kuwa na maji yaliyomwagwa na wanachama wa klabu hiyo (makomandoo) muda mfupi kabla ya timu hiyo kuwasili uwanjani.
    Kamati imeelekeza klabu ya Yanga iandikiwe barua ya onyo, na kuitaka kuhakikisha wanachama wake wanaacha mara moja mtindo wa kumwaga maji vyumbani baada ya kuwa vimeshafanyiwa usafi na wafanyakazi wa uwanja tayari kwa ajili ya matumizi ya timu yao. 
    Mechi namba 200 (Majimaji 4 vs Toto Africans 1). Katika mechi hiyo, timu ya Toto Africans ilifanyiwa vurugu ikiwa njiani kurejea hotelini baada ya mechi hiyo ambapo viongozi wake wawili waliumizwa. Tukio hilo liliripotiwa Kituo cha Polisi, na kesi tayari iko kortini. 
    Kituo cha Songea (Uwanja wa Majimaji) kiandikiwe barua ya kuhakikisha hazitokei vurugu uwanjani hapo baada ya mechi ikiwemo kuhakikisha timu ngeni inatoka uwanjani salama hadi kwenye hoteli ilikofikia. Iwapo vurugu zitaendelea, Bodi ya Ligi itasimamisha matumizi ya kituo hicho kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 9(2) ya Ligi Kuu.
    Aidha Kamati ilipitia matukio ya mchujo wa Ligi Daraja la Pili kuwania kwenda Daraja la Kwanza n mechi namba 7 (Mawenzi Market 2 vs Transit Camp 0). Klabu ya Transit Camp imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya timu yake kuchelewa uwanjani kwa dakika 45 katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 18, 2017 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. 
    Adhabu dhidi ya Transit Camp imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(1) na 14(47) kuhusu Taratibu za Mchezo. 
    Kocha Msaidizi wa Transit Camp, Thomas Gama amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutolewa nje na Mwamuzi katika mchezo kutokana na kumtolea maneno ya kashfa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja. 
    Mechi namba 8 (JKT Oljoro 1 vs Cosmopolitan 0). Klabu ya Cosmopolitan iliwasilisha malalamiko kuwa mechi hiyo iliyofanyika Machi 20,2017 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ilichezeshwa na Mwamuzi wa Arusha, badala ya Mwamuzi kutoka Singida aliyekuwa amepangwa awali. 
    Kamati imetupa malalamiko hayo kwa vile si ya kweli, na Mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo alitoka Mkoa wa Manyara, na si Arusha kama walivyodai katika malalamiko yao. 
    Mechi namba 12 (Transit Camp 1 vs Cosmopolitan 1). Daktari wa Cosmopolitan, Najim Mtoro amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kumtukana Mwamuzi wa Akiba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: POINTI TATU ZA CHEE SIMBA DHIDI YA KAGERA ZAWEKWA KIPORO, YANGA WAPEWA ONYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top