• HABARI MPYA

  Saturday, April 01, 2017

  SERENGETI BOYS YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI

  Na Mahmoud Zubeiry, BUKOBA
  TIMU ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kirafiki baada ya leo pia kuifunga Burundi 2-0 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Serengeti Boys baada ya juzi kuichapa Burundi mabao 3-0 katika mchezo mwingine wa kirafiki.
  Kocha Bakari Shime ‘Mchawi’ Mweusi anayefanya kazi chini ya Mshauri wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen leo alifanya mabadiliko makubwa kikosini mwake, akiwapa nafasi zaidi wachezaji ambao hawakucheza mechi ya kwanza.
  Abdul Suleiman Hamisi wa Serengeti Boys akimtoka beki wa Burundi leo Uwanja wa Kaitaba
  Kibwana Ally Shomari wa Serengeti Boys akimtoka beki wa Burundi
  Ibrahim Abdallah Ali wa Serengeti Boys akipambana na beki wa Burundi

  Nyota wa Serengeti Boys, Ibrahim Abdallah Ali (wa pili kulia) akipongezwa baada ya kufunga bao la pili leo

  Shukrani kwao wafungaji wa mabao ya Serengeti Boys leo, Issa Abdi Makamba dakika ya 36 na Ibrahim Abdallah Ali dakika ya 89.
  Serengeti Boys walitawala mchezo leo pamoja na wapinzani wao kucheza rafu nyingi na wangeweza kupata mabao zaidi kama wangekuwa makini zaidi kwenye kutumia nafasi walizotengeneza.  
  Serengeti Boys itaondoka kesho mapema kwa ndege kurejea Dar es Salaam ambako Jumatatu watakuwa na mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Ghana kabla ya kwenda Morocco kwenye kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na fainali za U-17 Afrika nchini Gabon Mei mwaka huu. 
  Kikosi cha Tanzania leo kilikuwa; Samuel Brazio, Issa Makamba, Kibwana Shomary, Cyprian Mtesigwa, Enrick Nkosi, Ally Msengi, Mathias Juan/Ally Ng'anzi, Marco Gerald/Israel Mwenda, Abdul Suleiman, Ibrahim Ali, Said Mussa/Asad Juma na Kelvin Kayego.
  Burundi; Djuma Bititateweho, Paul Amatungo, Djuma Ndayisenga, Blandin Muhimpundu, Omar Nzeyimana, Joel Noel Nzoyiha, Pierre Niyonkuru, Angelo Ruberintwari, Theodore Ngabirano na John Franck Nzojibwami.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top