• HABARI MPYA

    Monday, April 17, 2017

    MKWASA: HATUJAOMBA MSAADA WA FEDHA KWA MC ALGER

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KATIBU Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amekanusha madai kwamba ameomba msaada wa fedha kwa wenyeji wao, MC Alger ili waweze kuishi Algeria kwa siku nne baada ya kuachwa na ndege jana.
    “Watu wametafsiri vibaya nilichosema. Nilisema tutawasiliana na wenyeji wetu huku kujua namna ya kuishi kwa siku hizi nne. Sisi huku ni wageni, kuna sharia za kuishi nchi za watu, sisi tulikuja kwa ajili ya mechi, mechi imeisha tunabaki vipi, lazima wenyeji wetu watufanyie utaratibu,”. “Lakini pia tuna kundi kubwa la wachezaji huku na tukifika Dar es Salaam tuna mechi za mashindano, lazima tufanye mazoezi huku. Hivyo ndiyo maana nikasema tutawasiliana na wenyeji wetu kujua namna ya kuishi huku kwa siku hizi nne,”alisema Mkwasa leo akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa siku kutoka Algiers.   
    Charles Boniface Mkwasa (kuahoto) amekanusha madai kwamba ameomba msaada wa fedha kwa MC Alger ili waweze kuishi Algeria kwa siku nne baada ya kuachwa na ndege jana

    Wachezaji 11 wa Yanga SC pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa wamebaki mjini Algiers baada ya kuachwa na ndege kufuatia kuchelewa kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Algiers unaojulikana pia kama Uwanja wa Ndege wa Houari Boumediene jana.
    Wachezaji hao ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Beno Kakolanya; mabeki; Juma Abdul, Oscar Joshua, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kevin Yondan, viungo Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na mshambuliaji Donald Ngoma.  
    Na baada ya taarifa hizo baadhi ya vyombo vya Habari vikaripoti Yanga imeomba msaada kwa wenyeji wao, MC Alger.
    Kundi lingine la wachezaji wa Yanga limeondoka na ndege ya Emirates kurejea Dar es Salaam kupitia Dubai likiwa na wachezaji saba, ambao ni mabeki Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, viungo Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe kupitia Dubai.
    Katika kundi hilo kuna benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, Msaidizi wake, Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila pia wa Zambia, kocha wa makipa, Juma Pondamali, pamoja na Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.
    Wachezaji hao waliobaki sasa wataondoka Jumatano kwa ndege nyingine ya Uturuki na maana yake kambi ya Yanga sasa imegawanyika kuelekea mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Prisons Aprili 22. 
    Juzi Yanga ilitolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa mabao 4-0 na Mouloudia Club Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Al-Jaza’ir, Algiers, Algeria katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi.  
    Kwa matokeo hayo, Yanga inatolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam wiki iliyopita, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA: HATUJAOMBA MSAADA WA FEDHA KWA MC ALGER Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top