• HABARI MPYA

  Tuesday, April 18, 2017

  KUNDI LA MWISHO LA YANGA LAWASILI SALAMA DAR

  Na Steven Kinabo, DAR ES SALAAM
  WACHEZAJI 11 wa Yanga walioachwa na Ndege Nchini Algeria wakiongozwa na Katibu Mkuu Boniface Mkwasa wamewasili jioni ya leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
  Nyota hao ni Kelvin Yondani, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Deogratius Munishi ‘Dida’, Emmanuel Martin, Thabani Kamusoko, Andrew Vincent ‘Dante’, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Deus Kaseke na Benno Kakolanya, waliowasili pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa.
  Akizungumza baada ya kuwasili Dar ea Salaam leo, Mkwasa alisema kwamba walichelewa ndege kwa bahati mbaya kutokana na foleni za barabarani mjini Algires, lakini wanashukuru jitihada za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimewasaidia kurejea nyumbani mapema.
  Wachezaji hao walibaki mjini Algiers baada ya kuachwa na ndege ya shirika la Uturuki, kufuatia kuchelewa kufika Uwanja wa Houari Boumediene juzi.
  Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa (kulia) akiwa viungo wa timu hiyo Haruna Niyonzima na Deus Kaseke 

  Kundi lingine la wachezaji wa Yanga liliondoka juzi na ndege ya Emirates pia kurejea Dar es Salaam kupitia Dubai likiwa na wachezaji saba, ambao ni mabeki Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, viungo Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe.
  Kundi hilo lilikuwa na benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, Msaidizi wake, Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila pia wa Zambia, kocha wa makipa, Juma Pondamali, pamoja na Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.   
  Jumamosi Yanga ilitolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa mabao 4-0 na Mouloudia Club Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Al-Jaza’ir, Algiers, Algeria katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi.  
  Kwa matokeo hayo, Yanga imetolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam wiki iliyopita, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
  Kikosi kamili cha Yanga sasa kinaelekeza nguvu zake katika mashindano ya nyumbani na kwa kuanzia ni mecbi ya kiporo ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Tanzania Prisons Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga, Mabingwa watetezi wa Azam Sports Federation Cup wanawania kuungana na Simba, Mbao FC na Azam FC ambazo tayari zimetangulia Nusu Fainali.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KUNDI LA MWISHO LA YANGA LAWASILI SALAMA DAR Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top