• HABARI MPYA

    Wednesday, April 19, 2017

    KAMATI YA KATIBA YAAHIRISHA TENA KIKAO SUALA LA FAKHI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIKAO cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya sakata la beki Mohammed Fakhi kuichezea Kagera Sugar dhidi ya timu yake ya zamani, Simba akiwa ana kadi tatu za njano kipo shakani kufanyika leo.
    Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo baadhi ya watu waliowahitaji kutoa ushahidi wao mbele ya Kamati hawatapatikana leo.
    “Lakini pia sisi upande wa Kamati, safu yetu haiwezi kutimia kuna watu wana udhuru, kwa hivyo uwezekano wa kikao kuendelea leo ni mdogo sana, labda kesho,”alisema Mwesigwa.
    Kikao hicho kilichoanza Saa 4:00 asubuhi jana katika hoteli ya Protea, Masaki, Dar es Salaam kilifungwa Saa 2:05 usiku na Mwesigwa akasema kitaendelea leo kwa sababu wanahitaji vielelezo na ushahidi zaidi ili kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi.
    Kikao cha kujadili suala la Mohammed Fakhi (kulia) kipo shakani kuendelea leo  

    Kikao hicho kinafuatia Kagera Sugar kupinga uamuzi wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia timu hiyo kwa madai ya kumtumia Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
    Mwenyekiti wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki aliiomba TFF kupitia upya maamuzi ya Kamati ya Saa 72 kwa kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano kama ilivyodaiwa siku wanaifunga Simba 2-1.
    Ikumbukwe Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Utata upo katika mchezo wa Jumatano ya Januari 18, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kati ya wenyeji Kagera Sugar na African Lyon ya Dar es Salaam, ambao inadaiwa Fakhi alionyeshwa kadi ya njano wakati klabu yake inapinga.
    Viongozi wa klabu za Simba, African Lyon, Kagera Sugar, marefa na Fakhi mwenyewe walihojiwa jana Protea kwa nyakati tofauti na taarifa zinakinzana.
    Baadhi ya waliohojiwa wanasema kweli Fakhi alikuwa ana kadi tatu, lakini wengine wamesema mchezaji huyo hakuwa na kadi tatu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMATI YA KATIBA YAAHIRISHA TENA KIKAO SUALA LA FAKHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top