• HABARI MPYA

  Monday, April 10, 2017

  HIKI NDICHO LWANDAMINA ATAKIFANYA WIKI HII YANGA KUELEKEA MCHEZO WA MARUDIANO NA MC ALGER

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mzambia George Lwandamina amesema kwamba ataitumia wiki hii kurekebisha makosa aliyoyaona katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mouloudia Club Alger ya Algeria Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Yanga inarudi mazoezi leo kufuatia mapumziko ya kutwa jana, baada ya ushindi wa 1-0 juzi, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko dakika ya 61 akimalizia pasi ya kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa baada ya kazi nzuri ya kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima aliyepasua na mpira kutokea nyuma.
  George Lwandamina (wa pili kushoto) akiwa na wasaidizi wake, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila kulia kwake tu, Kocha wa Makipa, Juma Pondamali (kulia tu) na Kocha Msaidizi namba moja, Juma Mwambusi kushoto kabisa katika mchezo wa juzi dhidi ya MC Alger 
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana, Lwandamina alisema kwamba makosa madogo madogo atayafanyia kazi kuanzia leo, kubwa ni utumiaji wa nafasi. “Tulitengeneza nafasi nyingi, lakini tukatumia moja. Tunahitaji kutengeneza nafasi zaidi na kufunga mabao ya kutosha ili kujiweka salama,”alisema.
  Kwa ujumla Lwandamina alisema kwamba amefurahishwa na uchezaji wa timu yake juzi na sasa anaingia kwenye awamu ya pili ya maandalizi, kuelekea mchezo wa marudiano. “Akili yangu sasa naipeleka kwenye maandalizi ya awamu ya pili, natumai mambo yatakwenda sawa,”alisema.
  Yanga sasa itahitaji sare katika mchezo wa marudiano mwishoni mwa wiki hii mjini Algiers. Algeria ili kwenda hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho kwa mara ya pili mfululizo.
  Mwaka jana pia Yanga iliangukia kwenye kapu la kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kufuzu kwa kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola, kufuatia kutolewa na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HIKI NDICHO LWANDAMINA ATAKIFANYA WIKI HII YANGA KUELEKEA MCHEZO WA MARUDIANO NA MC ALGER Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top