• HABARI MPYA

  Wednesday, April 12, 2017

  CHIRWA AGOMA KUFANYA KAZI YANGA HADI ALIPWE MISHAHARA YAKE MITATU

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa amegoma kufanya kazi Yanga hadi alipwe malimbikizo ya mishahara yake ya miezi mitatu.
  Mgomo wa Chirwa umeanza rasmi leo baada ya kukataa kusafiri na timu kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Mouloudia Club Alger Jumamosi Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers.
  Yanga tayari imetoa orodha ya wachezaji 20 wanaoondoka kesho kwa ndege ya Emirates Air kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo huo na Chirwa hayumo ingawa sababu hazijatajwa.
  Katibu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema leo katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari kwamba, mbali ya Chirwa wengine ambao wataikosa ndege ya Emirates kesho kwa safari ya Algeria ni pamoja na Mzambia mwenzake, kiungo Justin Zulu ambaye ni majeruhi.
  Mzambia Obrey Chirwa hayumo kwenye kikosi cha wachezaji 20 wa Yanga wanaoondoka kesho kwenda Algeria 

  Wengine ambao hawaendi ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, beki Pato Ngonyani, kiungo Yussuf Mhilu na washambuliaji Malimi Busungu, Matheo Anthony.
  Japokuwa atakuwepo mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe, lakini wazi kukosekana kwa Chirwa kutamuumiza kocha Mzambia George Lwandamina, kwa sababu alicheza vizuri mechi ya kwanza na kuwasumbua mno mabeki wa MC Alger.
  Kikosi kamili kinachokwenda Algeria kesho ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Beno Kakolanya; mabeki; Juma Abdul, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Vincent Bossou, Kevin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
  Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Deus Kaseke, Geoffrey Mwashiuya na Emmanuel Martin wakati washambuliaji ni Donald ngoma na Amissi Tambwe pekee.  
  Yanga iliyoshinda 1-0 katika mchezo wa kwanza Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, inahitaji kwenda kulazimisha sare tu ugenini ili kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili mfululizo mwaka huu.
  Mwaka jana, Yanga pia ilicheza hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola ikitoka kutolewa na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa. 
  Yanga imepepesuka kiuchumi tangu Mwenyekiti wake, Yussuf Manji ambaye pia ni mfadhili kupata misukosuko na Serikali kuazia Janauri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHIRWA AGOMA KUFANYA KAZI YANGA HADI ALIPWE MISHAHARA YAKE MITATU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top