• HABARI MPYA

  Sunday, April 09, 2017

  ABDI BANDA ASIMAMISHWA KWA UBONDIA

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kati wa Simba, Abdi Banda amesimamishwa kwa muda usiojulikana kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla katika mchezo wa ligi hiyo baina ya timu hizo Aprili 2, Uwanja wa Kaitaba Bukoba.
  Hayo yamefikiwa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania au Kamati ya Saa 72, katika kikao chake cha juzi mjini Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo namba 194, ambao Kagera Sugar waliifunga Simba 2-1, Banda aliyekuwa amevalia jezi namba 24 amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri suala lake la kumpiga ngumi George Kavilla aliyevalia jezi namba 15 akiwa hana mpira kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Abdi Banda amesimamishwa kwa muda usiojulikana kucheza Ligi Kuu kwa kosa la kumpiga ngumi George Kavilla wa Kagera Sugar  

  Kama pia ilibaini Banda ambaye hakupewa adhabu yoyote na refa kwa sababu hakuona tukio hilo, alifanya kitendo cha aina hiyo kwenye mechi namba 169 kati ya Simba na Yanga iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam akimpiga kiungo Said Juma ‘Makapu’.
  Awali, Klabu ya Kagera Sugar iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.
  Kwa vile kosa hilo ni la kinidhamu, Kamati imemsimamisha Abdi Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9 (5) wakati akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Kamati ya Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
  Kamati ya Saa 72 pia imeagiza Daktari wa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Dk. Abel Kimuntu apelekwe Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu kutokana na kukataa kuwasilisha taarifa yake kuhusu tuhuma za kupuliziwa dawa kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Majimaji katika mechi namba 170 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya wenyeji Stand United. 
  Majimaji iliwasilisha malalamiko yake kwa Bodi ya Ligi kuhusu suala hilo na Kamati ikaagiza ripoti ya daktari huyo ambaye amekataa kutoa ushirikiano kwa mwendeshaji wa Ligi juu ya jambo hilo. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ABDI BANDA ASIMAMISHWA KWA UBONDIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top