• HABARI MPYA

    Tuesday, September 20, 2016

    SERIKALI YAIKUBALIA SIMBA SC KUREJESHA MECHI ZAKE UWANJA WA TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Habari Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye amesema kwamba Serikali pingamizi kwa Simba kurejesha mechi zake Uwanja wa Taifa kutoka wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Na Nape amesema kwamba wenye mamlaka ya kurejesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania za Simba Uwanja wa Taifa ni Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). “Sisi hatuna tatizo, wao wamalizane na Bodi ya Ligi na TFF,”alisema Nape akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.   
    Waziri Nape Nnauye (kushoto) akizungumza leo mjini Dar es Salaam
    Simba SC imeomba kurejesha mechi zake za Ligi Kuu Uwanja wa Taifa kutoka wa Uhuru, baada ya kubaini Uwanja wa Uhuru haupo vizuri.
    Katibu wa Simba SC, Patrick Kahemele alisema juzi mjini Dar es Salaam kwamba wachezaji wao watatu waliumia katika mchezo uliopita wakishinda 1-0 dhidi ya Azam FC Jumamosi kutokana na ubaya wa eneo la kuchezea la Uwanja wa Uhuru.
    “Vile vipira vya kwenye nyasi bandia pale uwanjani vimeharibika kutokana na kutotumika kwa muda mrefu, kwani vimepigwa jua, vimefubaa na kuwa kama vipande vya chupa, hivyo kuhatarisha usalama wa wachezaji wanapoanguka,”alisema Kahemele.
    Katibu huyo pia akasema Uwanja wa Uhuru ni mdogo ambao hauendani na mahitaji ya soka ya kisasa na kwamba hawatakuwa tayari kuutumia tena hadi hapo utakapokaguliwa na kuidhinishwa a wakaguzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    “Hatutaki na hatutoutumia Uwanja wa Uhuru hadi pale utakapofanyiwa marekebisha makubwa na kukaguliwa na wakaguzi wa CAF na FIFA,”alisema Meneja huyo wa zamani wa Azam FC.
    Pamoja na kuulalamikia Uwanja wa Uhuru, Simba SC imeshinda mechi zake zote ilizocheza hapo dhidi ya Ruvu Shooting 2-1, Mtibwa Sugar 2-0 na Azam 2-0.
    Katika mechi zake mbili za awali ilizocheza Uwanja wa Taifa, ilishinda moja 3-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara na kutoa sare ya 0-0 na JKT Ruvu. 
    Baada ya barua hiyo, sasa linasubiriwa tamko la Bodi ya Ligi juu ya wapi mchezo ujao wa Simba SC dhidi ya Maji Maji ya Songea utachezwa.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI YAIKUBALIA SIMBA SC KUREJESHA MECHI ZAKE UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top