• HABARI MPYA

  Sunday, September 18, 2016

  NGASSA KUKUTANA NA 'BOSI KUBWA' WA FANJA LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa leo anatarajiwa kuwa na kikao na Mwenyekiti wa klabu ya Fanja ya Oman, Sheikh Saif Abdullah Al-Sumri.
  Ngassa alitua Oman Alhamisi kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho ambayo kama yatakwenda vizuri, atajiunga na timu hiyo inayocheza Ligi ya Mabingwa ya Asia. 
  Na mchezaji huyo wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC, Azam FC na Simba za Dar es Salaam amekwenda y Oman, kiasi cha wiki mbili tangu avunje mkataba na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
  "Unajua huku kuanzia Ijumaa ndiyo mapumziko, watu hawafanyi kazi. Sasa mimi nilifika Alhamisi, ila Jumapili ndiyo nitakuwa na mazungumzo na Rais wa Fanja,”alisema Ngassa akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana kutoka Muscat, Oman.
  Mrisho Ngassa leo anatarajiwa kukutana na Mwenyekiti wa klabu ya Fanja nchini Oman, Sheikh Saif Abdullah Al-Sumri

  Ngassa alijiunga na Free State Stars Mei mwaka jana akisajiliwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne.
  Hata hivyo, kocha aliyemsajili baba huyo wa Farida (9) na Faria (7) alifukuzwa baada ya miezi miwili tu na sasa tayari yuko Mbeya City ya Tanzania.
  Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuwa Free State, Ngassa alifanya kazi na makocha wanne akiwemo huyu wa sasa, Mfaransa Denis Lavagne aliyeanza kazi Juni mwaka huu.
  Mwenyekiti wa klabu ya Fanja ya Oman, Sheikh Saif Abdullah Al-Sumri (kushoto)

  Wengine ni Mjerumani Ernst Middendorp aliyefanya kazi kati ya Septemba na Desemba 2015, Mtaliano Giovanni Solinas aliyefanya kazi kati ya Desemba na Mei 2016.
  Na Lavagne ndiye aliyechangia Ngassa kuomba kuondoka Free State baada ya kuonyesha kuidharau Tanzania haiwezi kuwa na mchezaji bora.
  Lavagne alimuanzishia benchi Ngassa katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya ABSA ya Afrika Kusini Agosti 23, kabla ya kumuingiza dakika ya 63 kwenda kuchukua nafasi ya Mbuyiselo Thethani wakati huo tayari FS imekwishapigwa 2-1, matokeo yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo.
  Na baada ya kuingia Ngassa akaenda kucheza kwa kiwango kizuri na kukaribia kufunga mara mbili hadi kocha huyo akampongeza baada ya mchezo, ingawa tayari mchezaji wa Tanzania alikwishatumbukiwa nyongo na Mfaransa huyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA KUKUTANA NA 'BOSI KUBWA' WA FANJA LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top