• HABARI MPYA

    Tuesday, September 20, 2016

    KILI QUEENS WAWANIA MWALI WA CHALLENGE LEO UGANDA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya taifa ya Tanzania Bara ya wanawake, Kilimanjaro Queens leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Ufundi, Njeru mjini Jinja, Uganda kumenyana na Kenya katika Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
    Kocha wa Kilimanjaro Queens, Sebastian Nkoma amesema kwamba anatarajia mchezo mgumu kwa sababu Kenya ni timu nzuri na imefuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake, ikiwa timu pekee katika ukanda wa CECAFA.
    Hata hivyo, Nkoma amesema kwamba wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kurejea na Kombe Dar es Salaam.
    “Tunataka kuweka rekodi ya kuwa mabingwa wa kwanza wa Challenge ya wanawake, japokuwa tunacheza na timu ngumu, Kenya. Tunajipanga kikamilifu kuhakikisha tunafanikisha hilo,”alisema kocha Nkoma akizungumza kutoka Jinja.
    Ikumbukwe, Kilimanjaro Queens iliingia fainali baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya wenyeji, Uganda, wakati Kenya iliifunga 3-2 Ethiopia.
    Awali, Tanzania Bara iliongoza Kundi B baada ya kushinda kura ya sarafu kufuatia sare ya 0-0 na Ethiopia katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo, hivyo kufungana nayo kwa pointi na wasatani wa mabao kileleni. 
    Kilimanjaro Queens ilianza vizuri michuano hiyo kwa kuibamiza 3-2 Rwanda, mabao yake yakifungwa na Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika za 11 na 65 na Stumai Abdallah dakika ya 28, wakati ya wapinzani wao yalifungwa na Ibangarrue Marie na Amina Ally wa Tanzania Bara aliyejifunga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILI QUEENS WAWANIA MWALI WA CHALLENGE LEO UGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top