• HABARI MPYA

    Tuesday, August 02, 2016

    ETI HUYU JAMAA NDIYE ANAIFANYA YANGA ‘IFUNGWE FUNGWE’ KOMBE LA SHIRIKISHO!

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    IMEELEZWA kwamba kufanya vibaya kwa Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kunasababishwa na kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Isaac Chanji.
    Chanji alijiuzulu baada ya uchaguzi wa klabu hiyo Juni 11, mwaka huu akitoa sababu za kubanwa na majukumu yake ya kazi Serikalini.
    Na aliondoka wakati Yanga inaingia kwenye mechi za Kundi A Kombe la Shirikisho, akitoka kumaliza msimu vizuri kwa kuiwezesha timu kushinda mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Isaac Chanji (kulia) akizungumza na Donald Ngoma (kushoto) baada fainali ya Kombe la ASFC wakiifunga Azam FC 3-1 

    Na tangu Chanji ameondoka Yanga, timu hiyo haijashinda mechi yoyote, ikifungwa tatu na kutoa sare moja kiasi cha kupoteza matumaini ya kwenda Nusu Fainali.
    Yanga ilifungwa 1-0 mara mbili, na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria na TP Mazembe Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Medeama SC mjini hapa na baadaye kwenda kufungwa 3-1 na timu hiyo nchini Ghana katika mchezo wa marudiano.
    Yanga itacheza mechi yake ya tano ya Kundi A na ya mwisho nyumbani Agosti 13, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia, mchezo ambao watahitaji lazima kushinda na baadaye wakashinde pia Lubumbashi dhidi ya DRC, ili kuangalia uwezekano wa kwenda Nusu Fainali.
    Na hiyo ni iwapo Medeama itafungwa na Mazembe na kwenda kutoa sare na Bejaia katika mechi zijazo.
    Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi nne, ikishinda tatu na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Bejaia na Medeama, ambazo kila moja na pointi tano za sare tatu na ushindi mmoja, wakati Yanga inashika mkia kwa pointi yake moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ETI HUYU JAMAA NDIYE ANAIFANYA YANGA ‘IFUNGWE FUNGWE’ KOMBE LA SHIRIKISHO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top