• HABARI MPYA

  Monday, May 09, 2016

  YANGA KUVUNA MILIONI 300 IKIWATOA WAANGOLA…NA BILIONI 1 INAWASUBIRI WAKITWAA KOMBE LA CAF

  ZAWADI KOMBE LA SHIRIKISHO...
  Nafasi za zawadi Mgawo wa YangaMgawo wa TFF
  Bingwadola 625 000dola 35 000
  Ikiingia fainalidola 432 000dola 30 000
  Ushindi wa pili wa kundidola 239 000dola 25 000
  Ushindi wa tatu wa kundidola 239 000dola 20 000
  Kufuzu hatua ya makundidola 150 000dola 15 000
  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itapewa kiasi cha dola za Kimarekani 150, 000 zaidi ya Sh. Milioni 300 iwapo itafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  TFF, Shirikisho la Soka Tanzania litapata mgawo wa dola 15,000 (Sh. Milioni 30 na zaidi) kutoka CAF kwa Yanga kuingia hatua ya makundi tu.
  Lakini dau hilo linaweza likapanda kwa Yanga hadi dola 239 (zaidi ya Sh. Milioni 500) na dola 20,000 kwa TFF (zaidi ya Sh. Milioni 40) iwapo timu hiyo itamaliza nafasi ya tatu katika kundi itakalopangwa.
  Na litapanda hadi dola 25,000 (Sh. Milioni 50 na zaidi) kwa TFF Yanga ikimaliza nafasi ya pili kwenye kundi. 
  Yanga ikiingia fainali itapata dola 432,000 (Sh. Milioni 870) wakati TFF itapewa dola 30,000 (Sh. Milioni 60 na zaidi).
  Ikifanikiwa kubeba Kombe la Shirikisho, Yanga itapewa dola 625, 000 (zaidi ya Sh. Bilioni 1.2), wakati TFF itapata dola 35, 000 (Sh. Milioni 700).
  Yanga inakaribia kutinga hatua ya makundi baada ya kuanza vyema katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua hiyo, baada ya kuifunga Sagrada Esperanca ya Angola Jumamosi mabao 2-0.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Yanga yalifungwa na wazawa Simon Msuva na Matheo Anthony na timu hizo zitarudiana Mei 17, mwaka huu Uwanja wa Sagrada Esperanca, zamani Quintalao do Dundo.
  Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
  Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
  Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUVUNA MILIONI 300 IKIWATOA WAANGOLA…NA BILIONI 1 INAWASUBIRI WAKITWAA KOMBE LA CAF Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top