• HABARI MPYA

  Tuesday, May 03, 2016

  YANGA INAPEPEA, NGOMA APIGA MBILI, TAMBWE MOJA… CHAMA LA WANA HOI!

  Na Prince Akbar, SHINYANGA
  YANGA imezidi kuusogelea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuafutia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Stand United jioni ya leo Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Ushindi huo ulitokana na mabao mawili ya washambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma na Amissi Tambwe wa Burundi, unaifanya Yanga ifikishe pointi 68 baada ya kucheza mechi 27.
  Yanga sasa inaweza kutangaza ubingwa ndani ya mechi mbili zijazo kati ya tatu za mwisho, iwapo itaendeleza wimbi la ushindi. 
  Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, Yanga tayari walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yote yakifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma.
  Ngoma alifunga bao la kwanza dakika ya pili kwa shuti kali, baada ya kuupitia mpira kwenye himaya ya mabeki wa Stand, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Assouman David.  
  Ngoma tena akawainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 45 kwa bao zuri akimlamba chenga kipa wa Stand United, Frank Muwonge baaada ya kutanguliziwa pasi nzuri na Mrundi, Amissi Tambwe.
  Kipindi cha pili, Yanga ilikianza vizuri tena na kufanikuwa kupata bao la tatu lililofungwa na Tambwe dakika ya 63 akimalizia kona ya winga Simon Msuva. 
  Elias Maguri akaifungia bao la kufutia machozi Stand United dakika ya 82 baada ya kiungo wa Yanga Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kumchezea rafu kiungo wa Stand, Suleiman Kassim 'Selembe'. 
  Yanga waliendelea kulisakama lango la Stand, lakini bahati yao leo ilikuwa ni 3-1.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan/Vincent Bossou dk66, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela/Mbuyu Twite dk46, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Deus Kaseke.
  Stand United; Frank Muwonge, Revocatus Richard, Selemani Mrisho, Nassor Masoud ‘Chollo’, Assouman David, Jacob Massawe, Vitalis Mayanga, Amri Kiemba, Elius Maguli, Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Salum Kamana/Pastory Athanas dk60. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA INAPEPEA, NGOMA APIGA MBILI, TAMBWE MOJA… CHAMA LA WANA HOI! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top