• HABARI MPYA

  Sunday, May 22, 2016

  WOTE WANGEKUWA KAMA DIDA…

  JUNI 24, mwaka jana kwa mara ya kwanza Charles Boniface Mkwasa alikutana na Waandishi wa Habari baada ya kuajiriwa kuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars katika Mkutano uliofanyika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam.
  Pamoja na kutaja benchi lake zima la Ufundi, Nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars akataja kikosi kipya, kutoka kile alichorithi kwa mtangulizi wake, Mholanzi Mart Nooij ambacho hakikuwa na matokeo mazuri.
  Na Mkwasa alimtema aliyekuwa kipa namba moja chini ya Nooij, Deo Munishi ‘Dida’, akiwachukua makipa watatu; Mudathir Khamis wa KMKM ya Zanzibar, Mwadini Ali wa Azam FC na Ally Mustafa ‘Barthez’ Yanga SC, zote za Dar es Salaam.

  Na Mkwasa aliyefanya mabadiliko makubwa akiwatema pia wakongwe wengine kama beki Erasto Nyoni na kiungo Mwinyi Kazimoto, alisema mabadiliko yake yamezingatia vitu mbalimbali, ikiwemo uwezo kushuka na umri mkubwa.
  Dida akarudi katika klabu yake, Yanga na kuendelea na bidii ya mazoezi na kujituma ili kupandisha tena kiwango chake.
  Na kwa sababu Barthez alikuwa katika kiwango kizuri wakati huo, hivyo Dida akawa kipa wa akiba Yanga kwa karibu msimu wote huu.
  Bidii ya mazoezi ya Dida ndani ya Yanga, ilimfanya hata kocha wa makipa wa timu hiyo, Juma Nassor Pondamali aseme makipa wake wote hao wawili wapo katika kiwango bora na yeyote anaweza kucheza.
  Usemi huo ukaja kuthibitika Aprili 9, mwaka huu baada ya Barthez kuumia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly Misri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushindwa kuendelea dakika ya 81 timu zikiwa zimefungana 1-1.
  Dida aliingia kwenda kumalizia mchezo ukaisha kwa sare ya 1-1 na akadaka pia mechi ya marudiano Cairo Yanga ikifungwa 2-1 na tangu hapo akawa anadaka hadi kuiwezesha Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Suala si kudaka tu, bali Dida amekuwa akidaka vizuri katika kipindi chote ambacho Barthez amekuwa majeruhi na ni uthibitisho kwamba ni kipa anayejitambua na anayejua wajibu wake pamoja na kuzikubali na mapitio tofauti.
  Na hata historia yake inaonyesha hivyo – kwani awali Dida akiwa kipa wa akiba anayelipwa vizuri Simba SC ya Dar es Salaam, aliamua kuondoka na kwenda Mtibwa Sugar kwenye maslahi kidogo na timu ya kijijini Manungu, ilia pate nafasi ya kucheza asiue kiwango chake.
  Akiwa Manungu akapata tena bahati, akasajiliwa timu ya mjini yenye kulipa vizuri, Azam FC ambako pia alikwenda kuwa kipa wa kwanza.
  Hata hivyo, akiwa Azam FC akaachwa ghafla na kwa bahati nzuri kwake akasajiliwa Yanga.
  Akiwa Yanga, Dida alikuwa kipa wa tatu nyuma ya Juma Kaseja na Barthez, lakini haikumkatisha tamaa, aliendelea na bidii hadi akafanikiwa kuwa kipa wa kwanza.
  Baadaye akaporwa namba na Barthez – lakini tena akakomboa namba na mwanzoni mwa msimu huu, akaporwa tena namba na kipa mwenzake huyo wa zamani wa Simba.
  Hakuna wakati Dida aliwahi kukata tamaa, siku zote amekuwa mchezaji mwenye kufanyia kazi mapungufu yake na ndiyo maana amekuwa akirudi katika ubora wake baada ya muda mfupi.
  Wazi baada ya kazi nzuri katika mechi za hivi karibuni, Dida ataendelea kudaka hata Barthez awe fiti kikamilifu kwa asilimia 100.
  Na anaweza pia kupewa jukumu la kulinda tena lango la Stars kwa kuwapiku Aishi Manula wa Azam FC na Beno Kakolanya wa Prisons alioitwa nao Stars.
  Wachezaji wote nchini wanapaswa kuwa kama Dida, kuzikubali changamoto na kuwa tayari kukabiliana nazo badala ya kukata tamaa au kutaka kupambana na maamuzi ya makocha.
  Natumia fursa yangu leo kumpongeza Dida na kumtaka aendelee vivyo hivyo – lakini pia kuwaambia wachezaji wengine nchini waige mfano huo.        
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WOTE WANGEKUWA KAMA DIDA… Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top