• HABARI MPYA

    Wednesday, May 04, 2016

    SIMBA SASA WANAKUMBUKA ZAMANI TU!

    HAJJI Sunday Manara ni Ofisa Habari wa Simba SC, ambaye ametoka kwenye mlango wa mahasimu wa jadi, Yanga SC.
    Hajji ni mtoto wa kuzaliwa na nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Manara enzi zake akiitwa Kompyuta.
    Sunday ni mdogo wa nyota mwingine wa zamani wa Yanga, Kitwana Manara ‘Popat’ ambaye alianza kama kipa baadaye akawa mshambuliaji tishio.
    Sunday ni kaka wa mchezaji mwingine wa zamani wa Yanga, Kassim Manara ambaye kama kaka yake huyo, (Baba Hajji) naye alifanikiwa kucheza Ulaya.
    Lakini hakuna shaka juu ya Usimba wa Hajji, kwani waliokuwa naye Kariakoo wanasema alianza kujipambanua tangu angali mdogo, kwamba amepishana na wazazi wake katika mapenzi ya timu.

    Kuzaliwa wakati baba zake wanacheza Yanga haikuwa kishawishi kwa Hajji kupenda timu hiyo ya Jangwani – yeye ni Simba, tena yule wa kulia.
    Hajji amekuwa kiongozi wa Simba katika kipindi hiki kigumu, ambacho timu haifanyi vizuri na kwa nafasi yake, anajikuta anakosa cha kuzungumza kuhusu maisha ya sasa ya klabu yake.
    Lakini kwa kuwa Hajji ni mzaliwa wa mjini, mwanasiasa na kada wa CCM aliyejaaliwa kipaji cha kuzungumza, basi haishiwi maneno.
    Sijui kama ni kumbukumbu alizonazo kwa sababu ametokea kwenye familia ya mpira, au anakwenda Maktaba kupekua pekua, lakini kwa sasa Hajji anawakumbusha sana wapenzi wa timu hiyo makali ya timu hiyo enzi hajazaliwa, anapakatwa au anachezea magari ya kusuka kwa waya au kutengeneza kwa maboksi.
    Ndiyo, Hajji leo anasimulia tukio la Simba la mwaka 1974 wakati kwanza alikuwa hajazaliwa na anaposimulia tukio la Wekundu hao wa Msimbazi, mwaka 1993 alikuwa ana umri gani?
    Lakini atafanya nini ikiwa wakati huu Simba haina ambacho mpenzi yeyote wa timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam atakipenda.
    Kufungwa na Yanga mechi zote za msimu, ama kufungwa na Coastal Union inayoshuka daraja au kufungwa na Toto Africans ambayo wachezaji wake wamezoea kufanya kazi bila mishahara, kipi atapenda kusikia mpenzi wa Simba?
    Kidogo labda tamthiliya ya ujenzi wa Bunju Complex, iliyoanza enzi Rais wa timu Alhaj Ismail Aden Rage na inaendelea wakati Rais ni Evans Elieza Aveva.
    Ndiyo maana sasa Hajji anajaribu kutofautiana kidogo na viongozi wengine wa Simba ambao wanafuatilia maisha ya mahasimu wao, Yanga na kuwaombea mabaya tu, kwa kuwapa simulizi tamu wapenzi wa timu hiyo kama zile za kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika 1974, kufika fainali ya Kombe la CAF 1993 na kuitoa Zamalek ya Misri katika Ligi ya Mabingwa 2003.
    Kuna nini tena – na inabidi sasa wapenzi wote wa Simba wawatambie mahasimu wao, Yanga kwa historia tu. 
    Kwani Yanga wamewahi kuitoa timu yoyote ya Kaskazini mwa Afrika (Waarabu) katika michuano yoyote ya Bara hili?
    Au Yanga zaidi ya kufika Robo Fainali ya Kombe la Washindi 1996 na Klabu Bingwa Afrika 1969, 1970 na 1998 wana nini zaidi cha kufikia rekodi ya mahasimu wao, Simba kwenye michuano ya Bara?
    Simba imefika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1974 na kutolewa kwa mbinde ne Mehallal El Kubra ya Misri.
    Simba imefika Fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa Stellah Abidjan. Simba wamecheza mechi kikombe cha Afrika kipo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kinawasubiri, bahati mbaya kikapakizwa kwenye ndege kwenda Abidjan baada ya Stella kushinda 2-0.
    Yanga lini wamecheza Kombe uwanjani michuano ya Afrika. Acha Simba  wajifariji kwa historia wakati huu, maana hakuna namna tena! 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SASA WANAKUMBUKA ZAMANI TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top