• HABARI MPYA

    Monday, May 09, 2016

    HANS POPPE: KUNA WACHEZAJI SIMBA WANATUMIWA KUUHUJUMU UONGOZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kuna kundi la watu wasiotakia mema klabu hiyo linawashawishi uovu wachezaji wa klabu hiyo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Hans Poppe amesema kwamba kundi hilo linawashawishi wachezaji kucheza chini ya kiwango na kuleta migomo baridi ili kuuchafulia uongozi uliopo madarakani.
    Kauli hiyo ya Poppe inafuatiwa baadhi ya wachezaji wa Simba SC kuegoma kwenda Songea kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Majimaji Jumatano.  
    Wachezaji saba wa Simba wakiwemo sita wa kigeni, wamegoma kusafiri kwenda Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Majimaji keshokutwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
    Hans Poppe amesema kuna wachezaji Simba wanatumiwa kuuhujumu uongozi

    Na sita wa kigeni, kipa Vincent Angban (Ivory Coast), mabeki Emery Nimubona (Burundi), Juuko Murshid (Uganda), viungo Justice Majabvi (Zimbabwe), Brian Majwega (Uganda), Hamisi Kiiza (Uganda) wamegoma kusafiri.
    Kiungo mkongwe, Mwinyi Kazimoto ni mchezaji pekee anayetumia hati ya kusafiria ya nyumbani aliyegoma kusafiri na wote ni kwa sababu moja, wamecheleweshewa mishahara ya Aprili.
    “Kuna msukumo unatoka nje ndiyo unafanya hivyo, maana mishahara kila mwezi huwa wanapata tarehe hizi, na hiyo ni kwa sababu wadhamini TBL (Kampuni ya Bia Tanzania) wanachelewa kutoa fedha hizo za mishahara,”amesema Hans Poppe.
    Hata hivyo, Poppe amesema tatizo la kuchelewa kwa mishahara kwa nchi hii si la Simba SC pekee, bali taasisi nyingi na hata timu nyingine kubwa za Ligi Kuu wachezaji hucheleweshewa mishahara na hawagomi.
    “Hapa kwetu kuna kidudu mtu, asi tulikwishajua siku nyingi, hata hizi mechi ambazo timu inafungwa au kutoa sare, si kwa sababu uwezo wa timu mdogo, kuna sumu za nje zinapenyezwa,”amesema Poppe.
    Hata hivyo, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba uongozi unalifanyia uchunguzi wa kina suala hilo kwa sasa na ukipata ushahidi wa kutosha utachukua hatua kali.
    “Kwa kweli tupo katika wakati mgumu, wakati tunapigania ustawi wa klabu, wengine wapo nje wanatusaliti kama hivi, unategemea nini kama si matokeo mabaya,”amesema. 
    Wakati Ligi Kuu inaelekelea ukingoni, Simba SC ikiwa imebakiza mechi tatu – tayari imepoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kufungwa 1-0 jana na Mwadui FC ya Shinyanga uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Matokeo ya jana moja kwa moja yanaipa ubingwa wa ligi hiyo Yanga SC yenye pointi 68 za mechi 27, ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.
    Aidha, Simba ilitolewa kimaajabu katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) baada ya kufungwa 2-1 na Coastal Union ya Tanga mjini Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE: KUNA WACHEZAJI SIMBA WANATUMIWA KUUHUJUMU UONGOZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top