• HABARI MPYA

    Monday, May 09, 2016

    AZAM NA YANGA FAINALI KOMBE LA TFF JUNI 11 TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    FAINALI ya kuwania Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) sasa zitafanyika Juni 11, 2016.
    Mchezo huo wa fainali utakaozikutanisha timu za soka ya Yanga na Azam FC utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba tarehe hiyo ni mwafaka kulingana na kalenda ya shughuli mbalimbali za soka.
    Alichambua ratiba na kalenda hiyo kuwa Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kufikia kikomo Mei 21, 2016 kabla ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuitwa kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ unaotarajiwa kufanyika Mei 29, mwaka huu.
    Taifa Stars itacheza mechi hiyo ikiwa ni maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Misri unaotarajiwa kufanyika Juni 4, 2016 jijini Dar es Salaam kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
    Tayari TFF imefafanua iwapo Bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu 2015/16 inayoendelea atashinda pia taji katika fainali za Kombe la Shirikisho la ASFC, ndiye atayeiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Afrika msimu wa 2016/17.
    Kwa msingi huo, timu itayopoteza fungwa katika fainali hizo za Kombe la Shirikisho –ASFC linalodhaminiwa na kituo cha Televisheni cha Azam, ndiyo itakayowakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika katika msimu wa 2016/17
    Fainali za Kombe la Shirikisho zinakuja baada ya mchuano ulioshindanisha timu 64 za Ligi Kuu Tanzania Bara - VPL (16); Ligi Daraja la Kwanza -FDL (24), Ligi Daraja la Pili – SDL (24).
    Wakati huo huo:  Kwa mara nyingine, Bodi ya Ligi Kuu imezikumbusha klabu zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2016/17 kuwa mchakato wa wa utengenezaji kanuni umeanza tangu Mei 5, 2016.
    Bodi ya Ligi kwa sasa inakaribisha maoni, mapendekezo, marekebisho kutoka klabu ili kuboresha uendeshaji wa ligi. Maoni hayo yanapokelewa kwa njia ya maandishi moja kwa moja kwenye ofisi za bodi au kwa njia ya barua pepe tplb.tplb@yahoo.com. Mwisho wa kupokea maoni hayo ni Mei 19, 2016.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM NA YANGA FAINALI KOMBE LA TFF JUNI 11 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top