• HABARI MPYA

  Sunday, April 03, 2016

  SAMATTA KAZINI TENA ULAYA LEO, ANAKIPIGA NA ANDERLECHT

  Na Somoe Ng’itu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta leo anatarajiwa kuichezea klabu yake, KRC Genk dhidi ya RSC Anderlecht katika mchezo wa Pro League utakaopigwa Uwanja wa Constant Vanden Stock mjini Brussels.
  RSC Anderlecht yenye mshambuliaji hatari Muargentina, Matias Ezequiel Suarez, itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa kwenye Uwanja wake huo wa nyumbani 1-0 Shakhtar Donetsk Machi 17, mwaka huu, wakati Genk mechi yake ya mwisho ilishinda 4-1 siku hiyo hiyo, dhidi ya KV Oostende, Samatta akifunga bao la kwanza. 
  Kwa wiki yote iliyopita, Samatta alikuwa Afrika kwa ajili ya ajili ya kuichezea timu yake ya taifa, Taifa Stars kwenye mechi za Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.

  Mbwana Samatta akishangilia baada ya kufunga katika ushindi wa 4-1 dhidi ya KV Oostende kwenye mchezo uliopita wa KRC Genk

  Na Nahodha huyo wa Tanzania alifanya kazi nzuri kwa kuifungia timu yake bao pekee kwenye ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji Chad mjini D’jamena wiki iliyopita.
  Hata hivyo, bahati mbaya ilikuwa ni kazi bure baada ya matokeo hayo kufutwa kufuatia Chad kujitoa na kusababisha hadi mechi ya marudiano isichezwe.
  Mchezo wa leo dhidi ya moja ya timu maarufu nchini Ubelgiji, RSC Anderlecht utakuwa wa saba kwa Samatta tangu ajiunge na Genk Januari mwaka huu akitokea TP Mazembe ya DRC, akiwa amefunga jumla ya mabao mawili. Kabla ya kufunga katika ushindi wa 4-1 dhidi ya KV Oostende, Samatta pia alifunga katika ushindi wa 3-2 baada ya kuingia dakika 15 za mwisho dhidi ya Club Brugge.
  Mechi nyingine alizocheza Samatta tangu atue Genk, zote akitokea benchi dakika za mwishoni ni dhidi ya Standard Liege (Genk) wakifungwa 2-1, dhidi ya Lokeren wakitoa sare ya 0-0, dhidi ya Waasland-Beveren wakishinda 6-1 na dhidi ya Mouscron-Peruwelz wakishinda 1-0 pia ugenini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA KAZINI TENA ULAYA LEO, ANAKIPIGA NA ANDERLECHT Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top