• HABARI MPYA

  Sunday, April 10, 2016

  PLUIJM: NIMEWAONA, TUNAKWENDA KUWAFUNGIA KWAO HAKUNA WASIWASI

  Na Somoe Ng’itu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema amewaona Al Ahly na kuanzia Jumatatu atawafanyia kazi ili akawang’oe kwao. 
  Yanga jana imelazimishwa sare ya 1-1 na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na kwa matokeo, Yanga watalazimika kwenda kushinda ugenini Aprili 19 ili kutimiza ndoto za kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili katika historia yao baada ya mwaka 1998.
  Han van der Pluijm (kulia) akijadiliana jambo na Meneja Hafidh Saleh wakati wa mchezo wa jana

  “Mchezo ulikuwa mgumu, Al Ahly ni timu bora, ni timu nzuri, lakini tunakwenda kufanyia kazi makosa yetu, ili tukawafunge kwao,”amesema Pluijm.
  Alipoulizwa kama hilo linawezekana kuwafunga Ahly kwao, Pluijm alisema; “Inawezekana, ondoa shaka. Hakuna jambo haliwezekani kwenye soka. Inawezekana. APR walipata matokeo kama haya (1-1) hapa, lakini tuliwafunga kwao. Na mwaka 2014 utakumbuka tulikaribia kuwatoa kwao Al Ahly,”.
  Pluijm amesema anawapa wachezaji wake mapumziko ya siku moja ya leo na Jumatatu wataanza maandalizi ya mchezo wa marudiano. 
  Katika mchezo wa huo, mabao yote yalipatikana kipindi cha kwanza, Ahly wakitangulia kufunga kupitia kwa mshambuliaji wake mjanja, Amr Gamal, kabla ya Yanga kusawazisha kwa bao la ‘ngekewa’ la Issoufou Boubacar.
  Gamal alifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ramadan Sobhi dakika ya 10, ambao uliwapita mabeki wote wa Yanga na kipa wao, Ally Mustafa ‘Barthez’ na kumkuta mfungaji pembeni ya lango akaujaza nyavuni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PLUIJM: NIMEWAONA, TUNAKWENDA KUWAFUNGIA KWAO HAKUNA WASIWASI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top