• HABARI MPYA

  Saturday, April 02, 2016

  PATACHIMBIKA CAMP NOU LEO USIKU NA EL CLASICO

  VIGOGO wa La Liga – Barcelona na Real Madrid za Hispania, zinakutana leo katika mechi ya 231 (El Clasico) kwenye Uwanja wa Camp Nou, mjini Barcelona.
  Wenyeji Barca, wakiwa jirani kutwaa ubingwa wa soka Hispania, wataingia dimbani wakiwa mbele kwa pointi 10 dhidi ya Madrid wanaoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo.
  Lakini pia, wanapambana na mahasimu wao katika soka la Hispania wakiwa na rekodi ya kutopoteza mechi kati ya 39 za mashindano yote.
  Kwa upande wa Real Madrid, wanashuka Camp Nou wakiwa na rekodi mbaya, kwani mara ya mwisho kupata usindi kwenye uwanja huo ilikuwa Aprili, 2012.

  Lakini pia, Los Blancos wana kazi moja kubwa ya kujaribu kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani - Bernabeu kwa kufungwa mabao 4-0 mwanzoni mwa msimum huu.
  Zikiwa zimebaki mechi nane kabla ya ligi kumalizika, Barcelona wanajidai kileleni wakiwa na pointi tisa dhidi ya wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo, Atletico Madrid.
  Hata hivyo, pengo linaweza kupungua hadi kufikia sita kama Atletico Madrid ataifunga Real Betis katika mechi itakayochezwa mapema leo.
  Na kama Real Madrid watafanikiwa kushinda mchezo wa leo, maana yake ni kwamba watatoa nafuu ya pengo la pointi kwao na majirani zao, Atletico Madrid.
  Kikosi cha Kocha Luis Enrique kililazimishwa sare ya 2-2 dhidiya Villarreal  katika mechi yao ya mwisho ya ligi kabla ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa.
  Sare hiyo ilimaliza kasi yao ya kucheza mechi 39 bila kupoteza. Hawajawahi kupoteza mechi tangu mwanzo wa Oktoba mwaka jana.
  Katika mechi 30 za La Liga, Barca wameshinda 24 na kupoteza mechi mbili tu. Wanashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi (86), wakitanguliwa na Real Madrid (87) na pia wana ngome bora iliyoruhusu mabao 24, wakiwa nyuma ya Atletico (14). 
  Sehemu kubwa ya mafanikio yao yametokana na muungano wa washambuliaji watatu - Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.
  Kawenye Uwanja wa Camp Nou, Barca wamecheza mechi 22 bila kupoteza mchezo, wakishinda mechi 20.
  Kadhalika, wamepoteza mchezo mmoja tu kati ya saba waliyocheza nyumbani kwa Real Madrid.
  Leo hii pia mechi hiyo itabeba taswira ya kumuenzi mkongwe wa Barceloba,  Johan Cruyff aliyefariki dunia mwanzoni mwa wiki hii kutokana na ugonjwa wa kansa. 
  Cruyff, raia wa Uholanzi alicheza Barcelona kati ya mwaka 1973 na 1978, kabla ya kuja kuwa kocha kwenye timu hiyo kati ya mwaka 1988 na 1996.
  Kwa upande wa Madrid, wana rekodi ya kutwaa mataji 32 ya La Liga kulinganisha na Barcelona waliotwaa mataji 23.
  Wana kazi kubwa ya kupambana na Barcelona na Atletico katika vita ya ubingwa wa Hispania. Timu hizi tatu zimekuwa bora kwa misimu kadhaa. 
  Real Madrid wameshinda mechi nne za mwisho za ligi wakiwa chini ya Zinedine Zidane ikiwa ni rekodi nzuri kwake tangu alipopoteza kwenye uwanja wa nyumbani kwa kufungwa bao 1-0 na Atletico.
  Kikosi hicho kiliandikisha ushindi katika mechi dhidi ya Levante, Celta Vigo na Las Palmas, kabla ya kuifunga Sevilla 4-0.
  Wachezaji, Gareth Bale na Karim Benzema, ambao kwa miezi ya karibuni walikuwa majeruhi, walirejea uwanjani na kujiunga na Cristiano Ronaldo. 
  Msimu huu, Real Madrid umepoteza mechi nne za ligi kwa kufungwa na Sevilla, Barcelona, Villarreal na Atletico.
  Lakini pia imeshinda mechi mbili tu za mwisho kati ya sita ilizokutana na Real Madrid msimu huu.
  Dondoo muhimu:
  Mechi ya leo itakuwa ya 231 (El Clasico), kati ya hizo, mechi 171 zimezikutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu (La Liga).
  Real Madrid ina rekodi nzuri ya kushinda mechi, ikifanya hivyo mara 71 na Barcelona imeshinda mechi 68.
  Katika mechi hizo, Real Madrid wamefunga mabao 278 na Barcelona mabao 272.
  Huenda timu leo zikapangwa hivi -
  Barcelona; 
  Bravo; Alves, Pique, Mascherano, Alba; Busquets, Rakitic, Iniesta; Neymar, Suarez, Messi.
  Real Madrid: 
  Navas; Danilo, Pepe, Ramos, Marcelo; Casemiro, Modric, Kroos; Ronaldo, Benzema, Bale. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PATACHIMBIKA CAMP NOU LEO USIKU NA EL CLASICO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top