• HABARI MPYA

  Friday, April 01, 2016

  NGASSA: YANGA WAKIJIAMINI WANAITOA AHLY

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa (pichani kushoto) amesema timu hiyo inaweza kuitoa Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kutoka Bethlehem, Afrika anakochezea klabu ya Free State Stars, Ngassa amesema kwamba kinachotakiwa ni wachezaji kujiamini.
  “Kama wachezaji watajiamini na kupambana kuanzia mwanzo hadi mwisho, tena kwa nidhamu ya hali ya juu, watawatoa (Ahly). Tatizo moja ambalo mimi nililigundua nilipokuwa pale Yanga, ni woga wa mechi,”.
  “Mara nyingi zinapowadia mechi kubwa kama hizi baadhi ya wachezaji huanza kuogopa timu, mnajikuta pamoja na maandalizi mazuri, lakini siku ya mechi mnacheza ovyo,”amesema Ngassa.
  Mrisho Ngassa alikuwepo kwenye kikosi cha Yanga kilichocheza na Ahly mwaka 2014

  Hata hivyo, Ngassa amesema anaamini baada ya Yanga kucheza na timu za Waarabu mfululizo miaka ya karibuni, anaamini hiyo itakuwa imesaidia kuondoa woga.
  Amesema kwamba na jambo la kufurahisha ni kwamba kikosi cha Yanga hakijabadilika sana, hivyo wachezaji tayari wanajua mbinu za Ahly na wanaweza kupambana nao.
  “Mimi ninaitakia kila heri tu timu yangu ya zamani, nawaamini wachezaji wenzangu niliokuwa nao pale hata wapya walioingia wanaweza kupigania heshima ya klabu na kuitoa Ahly,”amesema Ngassa.
  Yanga wanatarajiwa kuwa wenyeji wa Ahly Aprili 9, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya timu hizo kurudiana Aprili 19 mjini Cairo Misri.
  Mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, wakati timu itakayofungwa itaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. 
  Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2014 na Al Ahly ikaitoa Yanga kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake na Ngassa alikuwepo kikosini kabla ya kuhamia Free State msimu uliopita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA: YANGA WAKIJIAMINI WANAITOA AHLY Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top