• HABARI MPYA

    Wednesday, April 20, 2016

    MIPANGO YA ‘MWAKA 47’ NDIYO IMEIFELISHA SIMBA

    SIMBA SC ilitawala soka ya Tanzania mwanzoni mwa muongo uliopita hadi katikati.
    Wakati huo, kundi maarufu la wanachama wa klabu hiyo, Friends Of Simba lilikuwa likiisimamia timu na kuisaidia kwa hali na mali.
    Kundi hilo lilikuwa linafanya hivyo kwa kushirikiana na uongozi uliokuwa madarakani na hakuna siri- mafanikio ya klabu hiyo wakati huo yalitokana na wao.
    Hicho ndicho kipindi ambacho Simba SC iliwafunga watani wao, Yanga SC mfululizo mchana na usiku na kwenye mashindano yote.

    Hicho ndicho kipindi ambacho Simba SC ilitwaa mataji mengi mfululizo, kuanzia Ligi Kuu, Ligi ya Muungano, Kombe la FAT, Nyerere na hata Kombe la Kagame.
    Hicho ndicho kipindi ambacho Simba SC iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kuitoa kwenye mashindano timu ya Misri, baada ya mwaka 2003 kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek na kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 
    Lakini Friends walishindwa kuendelea na kazi yao nzuri waliyokuwa wakiifanya, baada ya kuingia uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage ambaye hawakuwahi kuiva naye chungu kimoja.
    Mambo yakawa magumu Simba SC wakati wa utawala wa Rage, hadi F.O.S. walipoamua kujipanga kuingia wao wenyewe madarakani.
    Awali walitaka kumsimamisha Zacharia Hans Poppe kugombea Urais, lakini ikatokea mizengwe wakaamua kumsimamisha Evans Eliaza Aveva ambaye alishinda.
    Julai 22, mwaka 2014 baada ya Aveva kuingia nadarakani, niliandika katika safu hii kuwaambia F.O.S. wanapaswa kufanya tathmini ya wakati ambao waliiwezesha klabu hiyo kutawala soka ya Tanzania na kufananisha na wakati huu, ambao Yanga na Azam wanatamba.
    Wanachama na wapenzi wa Simba SC walikuwa wana matumaini makubwa sana baada ya ushindi wa Aveva ambao ndio ushindi wa F.O.S.
    Niliwaambia uwezekano wa kutawala soka ya Tanzania kwa urahisi hivi sasa ni mgumu kwa sababu mambo yamebadilika tofauti na muongo uliopita.
    Wakati Friends wanaifanya Simba itawale soka ya Tanzania, Yanga SC ilikuwa timu hohe hahe haina uwezo wa kusajili wachezaji wazuri wala kocha wa maana, ama kuwalipa vizuri wachezaji au hata kufanya fitina nyingine za soka pamoja na maandalizi mazuri.
    Wachezaji wote wazuri walikuwa wanakwenda Simba SC na Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao waliachwa na timu zao, au kuita chipukizi kuwafanyia majaribio.
    Zaidi ya Yanga, timu nyingine iliyokuwa vizuri wakati huo ilikuwa Mtibwa Sugar, lakini nayo haikuonekana kuwa na dhamira ya kushindana kama ilivyokuwa siku za mwanzoni za ujio wake Ligi Kuu ilipoweza kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo 1999 na 2000.     
    Unaweza kuona Friends Of Simba walipita katika njia nyepesi mno kuifikisha Simba SC katika kilele cha mafanikio.
    Kwa sasa kuna Azam ni timu ya bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake wakati Yanga SC inajivunia Mwenyekiti wake, milionea Yussuf Manji.
    Yanga SC ya sasa si hohe hahe tena, inasajili wachezaji wa maana tena inaipiku Simba SC sokoni- inaajiri makocha wa maana, wachezaji wanalipwa na kuhudumiwa vizuri.
    Maandalizi ya timu yanakuwa mazuri kiasi cha kwenda hadi kuweka kambi Ulaya.
    Nikawaambia Friends Of Simba lazima waje kivingine, na mikakati na mbinu mpya ili wafanikiwe kuirudisha kwenye mstari Simba SC, lakini wakija na mawazo ya wakati ule walipoiwezesha timu kutawala kiulaini soka ya Tanzania, itakula kwao. 
    Leo ni takriban miaka miwili baadaye, Simba haijaweza kutwaa taji lolote la Ligi Kuu na hata msimu huu unaoelekea ukingoni tayari wenyewe wamekwishajikatia tamaa.
    Na Simba walijikatia tamaa baada ya kipigo cha Jumapili cha bao 1-0 kutoka kwa Toto Africans Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Na matokeo hayo yalikuja siku chache baada ya kutolewa na Coastal Union katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama ASFC.
    Simba ya Aveva sasa imekuwa ya kulalamika kila kukicha – wanaona wanaonewa kila siku na hii ni kwa sababu F.O.S. wanakutana na mazingira magumu ambayo hawakuzoea.
    Huu si wakati ule wa Yanga ya Mwenyekiti Francis Kifukwe na Katibu wake, Jamal Malinzi (sasa rais wa TFF) ambayo F.O.S. walikuwa wanaifunga Dar e Salaam, Morogoro, Arusha, Mwanza na Zanzibar. Sasa kuna Yanga ya Manji, inakwenda kambini Pemba, ikirudi Dar, inaua mnyama.
    Ligi Kuu ya sasa SI ile waliyokuwa wanaicheza kwa ustadi F.O.S. iliyokuwa ikiundwa na timu kama Milambo ya Tabora, Polisi Dodoma, AFC ya Arusha na Twiga ya Iddi Azzan- sasa kuna Azam FC, Mwadui FC na Mbeya City.
    Simba hawapaswi kulalamika chochote dhidi ya yeyote, wanapaswa kujilaumu wenyewe na mipango yao duni ya mwaka 1947 kuanzia kwenye usajili wa wachezaji hadi matunzo ya timu.
    Na wala katika hili sioni kama eti kuondoka kwa uongozi wa Aveva ndiyo jibu, bali ni wana Simba kuunganisha nguvu zao na kutafuta namna bora ya kuinasua klabu yao katika wakati huu mgumu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MIPANGO YA ‘MWAKA 47’ NDIYO IMEIFELISHA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top