• HABARI MPYA

  Tuesday, April 19, 2016

  MBIO ZA AZAM AFRIKA ZAISHIA TUNIS, YAGONGWA 3-0 NA ESPERANCE

  Na Princess Asia, TUNIS
  AZAM FC imeaga michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika baada ya kufungwa mabao 3-0 na wenyeji Esperance katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora usiku wa leo Uwanja wa Olimpiki Novemba 7 mjini Rades, Tunis, Tunisia.
  Matokeo hayo yanafanya Azam FC inayomilikiwa na bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake itolewe kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
  Ikicheza mchezo wa kujihami kwa kutumia viungo watano na mshambuliaji mmoja tu, Nahodha John Rapahel Bocco, Azam ilifanikiwa kuwabana vizuri wenyeji dakika 45 za kwanza na kumaliza bila kuruhusu bao.
  Nahodha wa Azam FC, John Bocco akiwafungva tela wachezaji wa Esperance leo Uwanja wa Olimpiki Novemba 7, mjini Rades, Tunis
  Kipa wa Esperance, Moez Ben Cherifia akidaka mpira wa juu dhidi ya mshambuliaji wa Azam, John Bocco
  Kiungo wa Azam FC, Ramadhani Singano 'Messi' akimtoka beki wa Esperance, Fousseny Coulibaly 

  Timu hiyo ya kocha Muingereza, Stewart John Hall ilikuwa ikifanya mashambulizi ya kushitukiza kwa kumpelekea mipira mirefu Bocco, ambaye hata hivyo alidhibitiwa.
  Ukuta wa Azam FC ulifanya kazi ya ziada ya kuzuia mashambulizi ya Esperance muda mwingi wa kipindi hicho, huku kipa Aishi Manula akiokoa michomo zaidi ya minne ya hatari langoni mwake.
  Hata hivyo, bao la mapema kipindi cha pili walilopata Esperance lilitibua mipango yote ya timu ya Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar esb Salaam.
  Bao hilo lilifungwa na Saad Bguir dakika ya 47 kwa shuti la mpira wa adhabu umbali wa mita 19, baada ya Fakhreddine Ben Youssef kuangushwa na David Mwantika nje kidogo ya boksi.
  Baada ya bao hilo, Azam FC walibadilisha mfumo na wao kuanza kushambulia moja kwa moja na hapo ndipo mchezo ukaanza kuwa pande zote.
  Hata hivyo, kufunguka kwa Azam FC kuliipa nafasi Esperance ya kufanikisha mipango yake na kufanikiwa kuongeza mabao mawili.
  Dakika ya 63 Haithem Jouini alifunga kwa kichwa akimalizia mpira uliotemwa na kipa Aishi Manula kufuatia krosi ya Hoiucine Regued na dakika ya 80 Fakhreddine Ben Youssef akafunga la tatu akimalizia pasi ya kiungo Driss Mhirsi.
  Azam haikuweza kabisa kulitia misukosuko lango la Esperance ambao walikuwa wanafurahia uchezeshaji wa marefa wa nchi jirani yao, Morocco.
  Kwa ujumla katika mchezo wa leo, Azam ilionekana kabisa kuathiriwa na kuwakosa wachezaji wanne tegemeo, mabeki Shomary Kapombe ambaye ni mgonjwa, Serge Wawa majeruhi, kiungo Jean Baptiste Mugiraneza aliyekuwa anatumikia adhabu ya kadi na mshambuliaji Kipre Tchetche aliyekuwa majeruhi pia. 
  Kwa matokeo hayo, Esperance itamenyana na moja ya timu nane zitakazotolewa katika 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Kikosi cha Esperance kilikuwa: Moez Ben Cherifia, Iheb Mbaarki, Yacine Rabii, Mohamed Ali Yaakoubi, Chamseddine Dhaouadi, Hoiucine Regued/Chaker Rergui dk87, Fousseny Coulibaly, Driss Mhirsi, Saad Bguir/Ilyes Jelassi dk77, Fakhreddine Ben Youssef na Haithem Jouini/Bernard Bulbwa dk83.
  Azam FC kipo; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum/Himid Mao dk79, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Ramadhani Singano ‘Messi’, Frank Domayo, John Bocco, Salum Abubakar ‘Sure Boy/Didier Kavumbangu dk79, Farid Mussa/Khamis Mcha dk65.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBIO ZA AZAM AFRIKA ZAISHIA TUNIS, YAGONGWA 3-0 NA ESPERANCE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top