• HABARI MPYA

  Wednesday, April 13, 2016

  MAYANJA ATAZAME AMESHIKAJE KISU KABLA YA KUENDELEA KUKIVUTA

  AMEKUWA na mwanzo mzuri, ni kweli – lakini haitakuwa ajabu wakati wowote uongozi wa Simba ukitoa taarifa za kushitukiza kwamba imetengana na kocha wake, Mganda Jackson Mayanja.
  Na Simba haitafanya hivyo kwa sababu inapenda, bali itafanya hivyo kwa sababu itajikuta inalazimika.
  Hiyo inatokana na maelewano ya kocha huyo na wachezaji kuendelea kuharibika kila kukicha.
  Hadi sasa, tayari Mayanja amekwishatofautiana na wachezaji wanne wa Simba SC na wawili wamefikia kusimamishwa, ambao ni mabeki Abdi Banda na Hassan Isihaka. Isihaka alitumikia adhabu yake, akamaliza na kurejeshwa kikosini, wakati Banda kwa sasa amesimamishwa.

  Huku hatima ya Banda ikiwa haijajulikana, Mayanja amewawekea kinyongo wachezaji wengine wawili, ambao ni Waganda wenzake, beki Juuko Murshid na mshambuliaji Hamisi Kiiza.
  Na Mayanja mwenyewe amekaririwa akisema kwamba Juuko na Kiiza ndiyo waliisababisha timu hiyo itolewe juzi Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kufungwa mabao 2-1 na Coastal Union katika mchezo wa Robo Fainali.
  Mayanja alisema kwamba uamuzi wake ya kuwaweka benchi wachezaji hao wa timu ya taifa ya Uganda ulikidhoofisha kikosi chake hata kikapoteza mchezo huo. 
  Lakini Mayanja amejitetea kwamba alilazimika kuwaweka benchi kutokana na utovu wao wa nidhamu na kutoheshimu majukumu yao kwenye timu.
  Kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Uganda, amesema kwamba amesema wachezaji hao walichelewa kuripoti kambini baada kuruhusiwa kwenda kuchezea timu yao ya taifa kwenye mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
  “Wachezaji wote (Juuko na Kiiza) wanastahili nafasi ya kucheza, lakini kwa mechi iliyotutoa Kombe la TFF nilishindwa kuwaweka kutokana na mimi kufuata taratibu, lakini kama wao ndiyo sababu ya kushindwa kwetu kwenye Kombe la TFF, basi wanapaswa kubeba lawama,”.
  “Naamini kila mchezaji anaweza kuchangia ushindi wa timu, Kiiza ni mfungaji anayeongoza katika Ligi, lakini nisingeweza kumpanga kwa sababu alikiuka taratibu za klabu baada ya kuruhusiwa kwenda kwenye mechi ya kimataifa,” alisema.
  Na ukirejea mchezo wa juzi ni kweli safu ya ulinzi ya Simba iliathiriwa na kumkosa Juuko na hata safu ya ushambuliaji ilikuwa butu kipindi cha kwanza, kwa sababu Kiiza hakuwepo.
  Kiiza aliingia kipindi cha pili na kuisawazishia Simba SC bao na kuwa 1-1 kabla ya Mcameroon, Youssouf Soba kukamilisha mabao yake mawili na kuipa ushindi wa 2-1 Coastal.
  Unaizungumzia Simba ambayo msimu huu inatafuta kwa udi na uvumba nafasi ya kurejea kwenye michuano ya Afrika, ikiwa ni miaka mitano tangu icheze kwa mara ya mwisho, Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Nafasi moja ya kurejea kwenye michuano ya Afrika kupitia michuano ya ASFC wamekwishaipoteza na sasa wanaendelea kujaribu bahati yao kwenye Ligi Kuu.
  Kwa sababu zile zile za kutafautiana na wachezaji, iwapo zitaendelea Simba haitapata inachokihitaji hata katika Ligi Kuu.
  Kama Mayanja anaamini Juuko na Kiiza walichangia Simba kutolewa na Coatsal – anadhani viongozi wa SImba watakuwa na mtazamo tofauti na huo?
  Ni kweli kwamba nidhamu ya wachezaji wa Tanzania si nzuri na wakati mwingine wamekuwa wakiwaambukiza hadi wachezaji wa kigeni.
  Lakini pamoja na ukweli huo, bado Mayanja anatakiwa kutafuta namna nyingine ya kuwarudisha wachezaji wa Simba kwenye mstari, badala ya hii anayoitumia sasa kwa sabubu mwisho wa siku itamgharimu mwenyewe.
  Ukiondoa Sir Alex Ferguson enzi zake Manchester Unted, hakuna kumbukumbu za kocha aliyeingia kwenye migogoro na wachezaji aliwahi kubaki kwenye timu.
  Hata ‘Special One’Jose Mourinho aliondolewa Chelsea kwa sababu ya wachezaji.
  Mayanja anawea kuwa kocha mzuri, lakini siku moja Simba hawatajali hilo na kumuambia awaachie timu yao, iwapo ataendelea kutunishiana misuli na wachezaji.
  Ni jambo rahisi sana, kama ni kisu Mayanja anatakiwa kuangalia ameshika upane upi, kwa sababu inaonekana yeye ndiye ameshika kwenye makali. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAYANJA ATAZAME AMESHIKAJE KISU KABLA YA KUENDELEA KUKIVUTA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top