• HABARI MPYA

    Sunday, April 03, 2016

    KIPA WA SIMBA AFUNGIWA MIAKA 10, GEITA GOLD NA POLISI ZASHUSHWA DARAJA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Wakil Jerome Msemwa leo imetoa maamuzi ya shauri la upangaji matokeo kwa mechi za Kundi C Ligi Daraja la Kwanza.
    Akisoma hukumu hiyo baada ya kumaliza kuwahoji viongozi wa klabu na Wenyeviti wa vya vyama vya mikoa husika jana, Wakili Msemwa amesema adhabu hizo zimetolewa kwa kufuata Kanuni za Nidhamu za TFF, na nafasi ya kukata rufaa kwa wahusika juu ya maaamuzi hayo ziko wazi.
    Klabu za Geita Gold (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) zimekutwa na hatia ya upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL) msimu ujao.
    Upande wa klabu ya JKT Kanembwa FC ya mkoani Kigoma, imeshushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL), baada ya kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa kundi lake, Kundi C.
    Kamati ya Nidhamu imewafungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh Mang’ola na kamisaa wa mchezo huo Moshi Juma baada ya kukutwa na hatia ya upagaji matokeo.
    Aidha kamati pia imemkuta na hatia kocha msaidizi wa klabu ya Geita Gold, Choke Abeid na kumfungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu
    Makipa Mohamed Mohamed wa JKT Kanembwa na Dennis Richard wa Simba anayecheza kwa mkopo Geita Gold, wamefungiwa miaka 10 kutojihusisha na mpira wa miguu sambamba na kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kila mmoja.
    Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Cosntantine Moladi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo.
    Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Yusuph Kitumbo, Katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa Tabora, Fateh Remtullah, Mwenyekiti wa klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernad Fabian wamefungiwa maisha kutojihusisha na mpira wa miguu.
    Mwamuzi wa mchezo kati ya Polisi Tabora v JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na mwamuzi wa akiba, Fedian Machunde wamefungiwa kwa muda wa miaka kumi kutojihusisha na mpira wa miguu, na kutozwa faini ya shilingi milioni (10,000,000) kumi kila mmoja.
    Katibu wa klabu ya Polisi Tabora, Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa klabu ya Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa timu ya Polisi Tabora, Mrisho Seleman, wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya kutokutwa na hatia.
    Kutokana na maamuzi hayo ya Kamati ya Nidhamu ya TFF, Kamati husika zitakaa kupitia Kanuni na kutangaza timu itakayopanda Ligi Kuu (VPL) msimu ujao na timu zitakazopanda Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
    Ikumbukwe Geita Gold, ambayo kocha wake Mkuu ni Suleiman Matola iliifunga mabao 8-0 JKT Kanembwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Polisi Tabora iliifunga 7-0 JKT Oljoro Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
    Na hayo yalitokea wakati Geita na Polisi zikiwa zimefungana kwa pointi Kundi C na timu ya kupanda kupanda Ligi Kuu ingepatikana kwa idadi ya mabao.
    Baada ya hapo, TFF ilitangaza kusitisha matokeo hayo na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi (Kamati ya Saa 72) iliyokutana Februari 16, mwaka huu kupitia taarifa za mechi hizo mbili ikalipeleka suala hilo Kamati ya Nidhamu kufuatia kutilia mashaka upangaji wa matokeo.
    Pamoja na hayo, Kamati ya Nidhamu ya TFF inazipa nafasi timu kukata rufaa.
    Na kwa mujibu wa kanuni, Mbao FC ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya nne ndiyo inayoapswa kuchukua nafasi ya kupanda Ligi Kuu, ingawa uamuzi rasmi utatangazwa na TFF wenyewe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPA WA SIMBA AFUNGIWA MIAKA 10, GEITA GOLD NA POLISI ZASHUSHWA DARAJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top