• HABARI MPYA

    Sunday, April 03, 2016

    ENYEAMA KUWANIA TENA TUZO YA MARC VIVIEN FOE

    KIPA wa Nigeria, Vincent Enyeama kwa mara nyingine ameteuliwa kuwania tuzo ya Marc-Vivien Foe katika orodha ya wachezaji 11 wa Kiafrika wanaocheza Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1.
    Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 33 ndiye kipa pekee aliyeingizwa kwenye orodha hiyo fupi pamoja na mabeki wawili, viungo watano na washambuliaji watatu.
    Mlinda mlango huyo wa Lille OSC atapambana wakali kama Serge Aurier, Abdul Majeed Waris, Moustapha Bayal Sall, Floyd Ayite, Ryad Boudebouz na Sofiane Boufal.
    Wengine walioingizwa kwenye orodha hiyo ni Rachid Ghezzal, Cheikh Noye, Cheick Diabate na mshambuliaji wa Cameroon, Benjamain Moukandjo.
    Kwa msimu huu, Enyeama amekuwa kivutio katika milingoti ya Lille akicheza jumla ya mechi 28, kati ya hizo, 12 akimaliza bila kuruhusu bao, akiokoa michomo 72, ikiwemo 45 aliyopelekewa kutoka ndani ya boksi.
    Mwaka 2014, Enyeama alichaguliwa Mchezaji Bora Mwafrika wa Ligi Kuu ya Ufaransa, baada ya kutoruhusu mabao katika mechi 14 za Lille, zikiwa ni jumla ya dakika 1,061 za kusimama langoni bila kufungwa, zikipungua 115 tu kufikia rekodi ya kipa wa zamani wa Bordeaux, Gaeten Huard ya kudaka mechi nyingi zaidi bila kufungwa daima Ufaransa mwaka 1993.
    Mshindi wa mwaka jana, Andre Ayew aliyembwaga Enyeama na Waafrika wengine, kwa sasa anachezea Swansea City ya England. Mshindi wa tuzo ya mwaka huu anatarajiwa kutajwa Mei mwaka huu.

    Vincent Enyeama kwa mara nyingine atawania tuzo ya Marc-Vivien Foe inayohusisha wachezaji wa Kiafrika wanaocheza Ligi Kuu ya Ufaransa, maarufu kama Ligue 1

    WANAOWANIA TUZO HIYO NI;
    Vincent Enyeama (Nigeria/Lille), Serge Aurier (Ivory Coast/PSG), Moustapha Bayal Sall (Senegal/Saint-Etienne), Floyd Ayité (Togo/SC Bastia), Ryad Boudebouz (Algeria/Montpellier), Sofiane Boufal (Morocco/Lille), Rachid Ghezzal (Algeria/ OlympiqueLyonnais), Cheikh Ndoye (Senegal/Angers), Cheick Diabaté (Mali/Bordeaux), Benjamain Moukandjo (Cameroon/FC Lorient) NA Abdul Majeed Waris (Ghana/FC Lorient).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ENYEAMA KUWANIA TENA TUZO YA MARC VIVIEN FOE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top