• HABARI MPYA

  Friday, March 04, 2016

  TWIGA STARS YAPIGWA 2-1 NA ZIMBABWE CHAMAZI

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  TANZANIA, Twiga Stars imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake baadaye mwaka huu Cameroon, baada ya kufungwa mabao 2-1 nyumbani na Zimbabwe jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Tanzania sasa itabidi ishinde ugenini kwa tofauti ya mabao mawili, au 2-1 ili mshindi aamuliwe kwa mikwaju ya penalti.
  Katika mchezo wa leo uliohudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Twiga Stars walianza vyema baada ya kutangulia kupata bao kupitia kwa kiungo wake mahiri, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ dakika ya 17 kwa shuti kali la mbali baada ya kupokea pasi ya Asha Rashid ‘Mwalala’.
  Stumai Abdallah wa Twiga Stars akimdhibiti Emmaculate Msipa wa Zimbabaw leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam

  Iliwachukua dakika mbili tu Zimbabwe kuchomoa bao hilo baada ya Erina Jeke kusawazisha kwa shuti la mbali dakika ya 19. 
  Mwanahimisi Gaucho alikaribia kufunga dakika ya 39 kama si shuti lake kutoka nje na dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
  Kipindi cha pili, Twiga Stars inayofundishwa na Nasra Juma ilirudi ikiwa dhaifu zaidi na kuwaruhusu wageni kutawala mchezo.
  Zimbabwe ‘waliwakera’ mamia ya Watanzania waliojitokeza Uwanja wa Chamazi baada ya kupata bao la pili dakika ya kwanza tu ya kipindi cha pili, mfungaji Erina Jeke aliyefumua shuti akimalizia krosi ya Majory Nyauwe.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Fatuna Omary, Stumai Abdallah, Maimuna Khamis/Fatuna Khatib dk73, Fatuma Issa, Annastazia katunzi, Donisia Minja, Happinnes Mwaipaja, Amina BIlali, Shlder Boniphace/Fatuma Makusanya dk21, Asha Rashid ‘Mwalala’ na Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’. 
  Zimbabwe; Chido Dzingirai, Felistus Muzingodi, Eunice Chibanda, Sheila makoto, Nobhule Majika, Luntet Mutokuto, Daisy Kaitano/Rejoice Kapfuvuti dk75, Emmaculate Msipa, Majory Nyauwe, Erina Jeke/Mavis Chirandu dk79 na Rudo Neshamba/Patience Mujuru dk90.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TWIGA STARS YAPIGWA 2-1 NA ZIMBABWE CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top