• HABARI MPYA

  Wednesday, March 02, 2016

  TAIFA STARS KUIVAA CHAD BAADA YA MAZOEZI YA SIKU MBILI

  Na Renatha Msungu, DAR ES SALAAM 
  TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars itakuwa na kambi ya mazoezi ya siku mbili kabla ya mechi mbili mfululizo za Kundi G nyumbani na ugenini dhidi ya Chad ndani ya tatu kuwania tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2017. 
  Machi 25 mwaka huu, Taifa Stars itamenyana na wenyeji, Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya mjini N'Djamena katika mchezo wa Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017 nchini Afrika Kusini kabla ya timu hizo kurudiana Machi 28, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kikosi cha Taifa Stars

  Akizungumza na Lete Raha, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ambaye timu yake imeambulia pointi moja katika mechi mbili za kwanza za kundi hilo, baada ya kufungwa ugenini 3-0 na Misri na kulazimishwa sare ya 2-2 na Nigeria Dar es Salaam, Mkwasa alisema wamekosa muda wa maandalizi zaidi kutokana na wachezaji kubanwa na klabu zao.
  Mkwasa amesema safari hii imekuwa vigumu kuweka kambi ya muda mrefu kutokana na wachezaji kubanwa na klabu zao, ambazo zitakuwa kwenye mashindano tofauti mfululizo.
  Hata hivyo, Mkwasa amesema kwa klabu ambazo zina wachezaji walio kwenye mipango yake ya mechi hizo amezungumza na makocha wao na kuwapa programu za mazoezi ya ziada ya kuwapa vijana hao kabla ya kujiunga na kambi ya Stars kwa michezo dhidi ya Chad.
  “Kwa mfano Yanga na Azam ambazo zote zinacheza michuano ya klabu Afrika, zote zitakuwa na mechi Machi 11 na baada ya hapo watakuwa na mechi ya marudiano wiki moja baadaye, kwa hivyo siyo rahisi kuwaita kambini,”amesema. 
  Baada ya mechi za Chad, Taifa Stars itacheza nyumbani na Misri kabla ya kusafiri kwenda Nigeria kwa mchezo wa mwisho wa kundi hilo, kasha kuangalia mustakabali wake wa kufuzu.
  Ikumbukwe kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za Mataifa ya Afrika mwaka 1980, ambako iliishia hatua ya makundi baada ya kufungwa 3-0 na wenyeji, 2-1 na Misri na sare ya 1-1 na Ivory Coast.
  Mara ya mwisho Tanzania kukutana na Chad yenye wakali kama Ezechiel N'Douassel wa Sfaxien ya Tunisia, Rodrigue Ninga wa Montpellier ya Ufaransa, Marius Mbaiam wa Belfort ya Ufaransa, Leger Djime anayechezea klabu ya nyumbani kwa sasa, Foullah Edifice baada ya kuchezea Al Nasr ya Misri na Difaa El Jadida ya Morocco, Mahamat Labbo wa R.O.C. de Charleroi-Marchiennena ya Ubelgkji na Karl Max Barthelemy wa  Difaâ El Jadidi  ya Morocco, ilikuwa mwaka 2014.
  Ilikuwa ni katika mchujo wa kufuzu Kombe la Dunia, Raundi ya kwanza na Taia Stars ikakitoa Chad kwa mbinde, ikifungwa 
  1-0 nyumbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushinda 2-1 mjini N'Djamena, hivyo kusonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla 2-2. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS KUIVAA CHAD BAADA YA MAZOEZI YA SIKU MBILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top