• HABARI MPYA

  Wednesday, March 02, 2016

  SHERIA NAMBA MOJA IMESIGINWA, HIZO NYINGINE VIPI?

  SHERIA namba moja katika sheria 17 za soka ni; Eneo la kuchezea (The Field of Play), ambayo inasema soka lazima ichezwe katika Uwanja wa nyasi ama halisi, au za bandia, lakini mwonekano lazima uwe rangi ya kijani.
  Eneo la kuchezea mpira linapaswa kuwa katika mwonekano mzuri, wenye kuonyesha alama zote nyeupe za kuyagawa maeneo ya Uwanja na magoli yote mawili. 
  Kwa Tanzania, suala la Uwanja halipewi kipaumbele na akabu hiyo ndiyo sharia namba noma ya soka.
  Ndiyo maana zaidi ya miaka 80 sasa klabu kongwe kama Simba na Yanga hazina viwanja na eti hizo ndizo zinategemewa zichangie kwa kiasi kikubwa maendeleo ya soka yetu.

  Mapema wiki hii nimeshuhudia mchezo wa hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliofanyika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi kati ya wenyeji Panone FC na Azam FC ya Dar es Salaam iliyoshinda 2-1 na kwenda Robo Fainali.
  Mapema tu kabla ya kuanza kwa mchezo, nilijiuliza Uwanja wa Ushirika unaruhusiwa vipi kutumika si kwa mashindano makubwa kama Kombe la TFF, bali mashindano yoyote ya soka ya ngazi yoyote, hata Daraja la 10 kama lipo.
  Sehemu kubwa ya Uwanja haina nyasi, maana yake mchezaji akianguka tu au kuteleza hawezi kuepuka jeraha kubwa. Na bahati mbaya zaidi, kwenye kikosi cha Azam FC kulikuwa kuna wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars ambayo baadaye mwezi huu itacheza mechi mbili mfululizo ndani ya siku tatu za Kundi G dhidi ya Chad kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
  Sahau kuhusu wachezaji wa Azam FC ambao tunawategemea katika kampeni hiyo ya kufuzu AFCON ya mwakani, lakini kila mchezaji hata wa Panone wana haki ya kucheza katika mazingira salama, ilikuwaje TFF ikaruhusu mchezo huo ufanyike kwenye Uwanja hatarishi namna ile?
  Hakuna sababu ya kucheza mpira kwenye Uwanja ‘kipara’ na ni bora tuache tu kabisa kucheza na tuchague michezo mingine kama drafti au bao, ikiwa soka imetushinda.
  Najaribu kujiuliza viongozi wa soka ambao wameshindwa kuheshimu sheria namba moja ya mchezo watatushawishi vipi tukubali wataheshimu sheria nyingine za soka? Inastaajabisha marefa ambao wameshindwa kuheshimu sheria namba moja ya soka wakaweza kusimamia nyingine 16!
  Hii inanifanya nianze kuamini kama Watanzania wengi wanavyoamini kwamba mpira wa miguu nchi hii hautaendelea milele kwa sababu bado hatujapata viongozi sahihi, kuanzia ngazi za klabu, wilaya, mikoa na taifa.
  Tumeifanya soka yetu yote kuwa ni ‘ndondo’ tu tunaitumia ili kuganja njaa tu na si kucheza kwa malengo ya siku moja kufika katika hatua fulani.
  Haiyumkiniki TFF kuruhusu mpira kuchezwa kwenye Uwanja usio na nyasi kwa kisingizio chochote, kwa sababu nyasi zinaoteshwa tu. Wameweza kuingia gharama za kujenga uzio na majukwaa kwa gharama za mamilioni mengi, kwa sababu tu waweze kuingiza watu kwa malipo, lakini wameshindwa kutumia gharama kidogo na muda kuotesha nyasi.
  TFF wanatumia nguvu nyingi kwenye mambo mengine ambayo kimsingi hayana uzito wa kufikia hili la sheria namba moja ya soka, kama inavyoanishwa na wenye mpira wao, FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa).
  TFF wanaweza wakaniambia, kama wameshindwa kuheshimu sheria namba moja ya soka, tuamini vipi wataweza kuheshimu nyingine 16? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHERIA NAMBA MOJA IMESIGINWA, HIZO NYINGINE VIPI? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top