• HABARI MPYA

  Tuesday, March 01, 2016

  SAMATTA AINGIZWA KWENYE GAME YA PLAYSTATTION FIFA 16

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAKATI Watanzania wakisherehekea mchezaji ‘kipenzi chao’ Mbwana Ally Samatta kufunga bao la kwanza tangu aanze kucheza Ulaya – kuna habari mpya nzuri kuhusu mshambuliaji huyo wa KRC Genk ya Ubelgiji.
  Ipi hiyo? Samatta amejumuishwa kwenye kikosi cha Genk katika game ya playstation ya FIFA 16 na huo mwendelezo wa mafanikio yake tangu msimu uliopita.
  Tayari mashabiki wa soka wameanza kumchezesha mchezaji huyo akiwa na kikosi cha Genk na jezi yake namba 77 anayovalia.
  Ikumbukwe Samatta alijiunga na Genk kwa dau la Euro 800,000 akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe pamoja na kuwa mfungaji wa michuano hiyo na pia kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika ya CAF.
  Mbwana Samatta akifunga bao lake la kwanza Ulaya Jumapili

  Na tangu ametua Genk amekuwa akicheza kila mechi, japokuwa anatokea benchi na katika mchezo wake wa tatu tu, amefunga bao la kwanza.
  Samatta alifungua akaunti yake mabao katika klabu yake mpya, KRC Genk katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji Jumapili jioni wakishinda 3-2 dhidi ya Club Bruge Uwanja wa Cristal Arena, Genk.
  Samatta aliyejiunga na Genk Januari akitokea TP Mazembe ya DRC, alifunga bao hilo dakika ya 81 akimalizia pasi ya kiungo Ruslan Malinovskiy, baada ya kuingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Nikolaos Karelis dakika ya 79.
  Samatta akifurahia na wachezaji wenzake kwenye chumba cha kubadilishia nguo baada ya mechi Jumapili
   

  Mabao mengine ya Genk siku hiyo yalifungwa na Karelis kwa penalti dakika ya 36 na Thomas Buffel dakika ya 50, wakati ya Bruge yamefungwa na Thomas Meunier dakika ya 15 na Hans Vanaken dakika ya 83.
  Na ushindi huo, unaifanya Genk ifikishe pointi 45 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kukamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AINGIZWA KWENYE GAME YA PLAYSTATTION FIFA 16 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top