• HABARI MPYA

  Wednesday, March 09, 2016

  NGASSA ‘AUMIA VIBAYA’ AFANYIWA OPERESHENI NA ATAKUWA NJE ZAIDI YA MIEZI MIWILI

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MCHEZAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa atakuwa nje kwa miezi miwili au zaidi, baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu jana.
  Ngassa aliumia wiki iliyopita katika mchezo wa Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini wiki mbili zilizopita na baada ya vipimo ikaonekana anahitaji kufanyiwa upasuaji.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana kwa simu kutoka Afrika Kusini, Ngassa alisema kwamba maumivu hayo ndiyo yamemsababisha hata asiorodheshwe kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  Mrisho Ngassa atakuwa nje ya Uwanja kwa zaidi ya miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji jana
  Ngassa ameomba Watanzania wamuombee dua apone haraka na kurejea uwanjani
  Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa jana ametaja kikosi cha wachezaji 25 bila kumuorodhesha Ngassa anayechezea Free State Stars ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
  Na kiungo huyo amesema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilituma barua kwa klabu yake kumuombea ruhusa ya kurejea nyumbani kujiunga na Taifa Stars, lakini wakaambiwa hali halisi.
  “Free State wamewaambia TFF kwamba mimi ni majeruhi, kwa hivyo sitakuwepo katika timu safari hii. Lakini nitakosekana kwa muda mrefu tu, naomba Watanzania waniombee dua nipone nirudi kazini,”amesema Ngassa ambaye yupo katika msimu wake wa pili Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini tangu ajiunge na Free State kutoka Yanga ya nyumbani, Tanzania.
  Kikosi kamili cha Stars alichotaja Mkwasa jana kwa ajili ya mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Chad kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017 baadaye mwezi huu kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Azam FC), Ally Mustapha (Yanga SC) na Shaaban Kado (Mwadui FC), mabeki; Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kevin Yondani (Yanga SC), Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika (Azam FC) na Mohamed Hussein (Simba SC).
  Viungo; Himdi Mao (Azam FC), Ismail Juma (JKU), Jonas Mkude, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto (Simba SC), Mohammed Ibrahim, Shizza Kichuya (Mtibwa Sugar), Farid Mussa (Azam FC), Deus Kaseke (Yanga SC).
  Washambuliaji; Mbwana Samatta (Nahodha, KRC Genk Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), John Bocco (Azam FC), Elias Maguri (Stand United), Jeremia Mgunda (Tanzania Prisons) na Ibrahim Hajib (Simba SC).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA ‘AUMIA VIBAYA’ AFANYIWA OPERESHENI NA ATAKUWA NJE ZAIDI YA MIEZI MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top