TIMU ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC yamefungwa na mshambuliaji Suleiman Abdallah Mwalimu ‘Gomez’ dakika ya 37 na winga Msenegal, Libasse Guèye dakika ya 45’+2.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 22 katika mchezo wa tisa na kusogea nafasi ya nne ikizidiwa tu wastani wa mabao na mabingwa watetezi, Yanga SC ambao pia wana mechi moja mkononi.
Kwa upande wao KMC FC baada ya kupoteza mchezo huo wanakamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu wakiwa mkiani wakibaki na pointi zao nane za mechi 15 kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment