• HABARI MPYA

  Wednesday, March 09, 2016

  HAKUNA HAJA YA KUUMIZA KICHWA KUFIKIRIA, NI MALINZI TU!

  KWA kiasi kikubwa na kwa muda mrefu Watanzania wengi wamekata tamaa na soka ya nchi yao na wengi wamekwishajitoa kabisa na kubaki wanashabikia soka ya Ulaya.
  Ushabiki na mapenzi makubwa yaliyobaki ni kwa Simba na Yanga tu na ambazo watu wanazipenda huku wakizichukia.
  Wanazipenda ni timu zao, lakini zinawaudhi kwa sababu hazibadiliki na hazina mwelekeo wenye kueleweka.
  Lakini kama walivyosema wahenga, damu nzito kuliko maji, inapotokea soka ya Tanzania ikaonyesha mwamko kidogo, watu hurejesha mapenzi.

  Na kwa sababu hiyo, Watanzania wachache wenye mioyo ya ujasiri kidogo hukubali hata kujitokeza kujibebesha dhamana ya kujaribu kuikwamua soka ya nchi hii.
  Bahati mbaya sana, wachache huwa na dhamira ya kweli ya kutaka kuikwamua soka ya nchi yetu, lakini wengi hutaka kuitumia kama ngazi au daraja la kuwavushia kwenye maslahi yao mengine.
  Ndiyo maana unaweza kuona leo umaarufu wa wanasiasa wengi nchini umeanzia kwenye soka – na sioni sababu ya kuwataja, kwa sababu wanajulikana.
  Kwa kujua soka ni mchezo unaopendwa na wengi, ni rahisi kuteka hisia za watu na kujipatia umaarufu, hatimaye kwenda kutimiza malengo yao mengine watu wamekuwa wakiitumia kufanikisha mipango yao mingine.  
  Lakini bado wapo viongozi wachache wenye dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko katika soka yetu – ila tu bahati mbaya wanakwamishwa na mambo kadhaaa ambayo ukiyatafakari inakatisha tamaa.
  Unakuta kiongozi kachaguliwa pamoja na watu wa kambi nyingine, ambao bado wanaendelea kutamani siku moja wawe madarakani na washirika wao.
  Nitafafanua kidogo hapa, mfano katika kampeni mgombea Umakamu alikuwa pamoja na mgombea Urais ambaye hakupita – mara nyingi huyo huwa ni vigumu kutoa ushirikiano kwa mwenzake.
  Zaidi atafanya jitihada za kumhujumu aonekane amefeli na siku moja watu waseme; “Fulani hafai” au “Kashindwa”.
  Sitaki kusema hii ndiyo picha halisi katika soka letu kwa sasa, hapana. Naamini, pale TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) watu wote ni wamoja na wanafanya kazi kwa ushirikiano wa kutosha.
  Lakini Napata wasiwasi namna Rais wa TFF, Jamal Malinzi anavyonyooshewa kidole yeye binafasi kwa karibu kila jambo linalokwenda tofauti na matarajio.
  Wahenga wanasema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni – Malinzi amejitahidi sana kwa kipindi kifupi alichokaa madarakani kufanya mambo yenye manufaa kwa mustakabali wa soka ya Tanzania.
  Ametilia mkazo uwekezaji kwenye soka ya vijana na amekuwa na programu rasmi iliyobeba dira ya maendeleo ya soka ya nchi hii, ambayo utekelezaji wake unaendelea.   
  Lakini ajabu hata refa akivurunda katika uchezeshaji wake lawama atatupiwa Malinzi.
  Azam FC ikiruhusiwa kwenda kwenye michuano ya kirafiki Zambia wakati Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea, lawama atatupiwa Malinzi.
  Simba SC ikimtumia Ibrahim Hajib wakati ana kadi kadi tatu za njano, lawama atatupiwa Malinzi.
  Charles Boniface Mkwasa akimvua Unahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kumpa Mbwana Ally Samatta, lawama atatupiwa Malinzi.
  Watu hawapati tabu, hawajisumbui hata kufikiria, wamekwishakariri kumsukumia lawama Malinzi – hata Twiga Stars ikifungwa. Malinzi huyo.
  Kinachosikitisha zaidi hata sisi Waandishi wa Habari tumeingia kwenye siasa za majungu na badala ya kuitumia taaluma yetu kusaidia maendeleo ya mchezo, tunatumika kuharibu mambo.
  Ligi Daraja la kwanza kwa mara ya kwanza kihistoria ina udhamini, mikataba ya udhamini ya Ligi Kuu yote ya Azam TV na Vodacom imeboreshwa. Kombe la TFF limerudi likiwa na udhamini pia.
  Ushindani katika Ligi Kuu umeongezeka na idadi ya timu zimeongezeka pia. Malinzi ana kawaida ya kufanyia kazi mambo kwa haraka na tumeona mara kadhaa akichukua hatua za haraka juu ya kero mbali mbali.
  Lakini pia ni mtu ambaye anawashirikisha wadau, mfano wa vyombo vya habari, kiasi cha kuanzisha umoja wa mawasiliano kwenye mitandao ya jamii baina yake na Wahariri wa Michezo. Wakati mwingine tunapaswa kuunga mkono juhudi tunazoziona zina mlengo wa mafanikio ili kujijengea imani mbele ya jamii inayotuzunguka.
  Martin Luther King Jr. aliwahi kusema; “You do not have to see the whole staircase. Just take the first step,”, yaani ukitaka kupanda ngazi ndefu, huhitaji kuziona ngazi zote ili kufika juu. Anza na ile ngazi ya kwanza na panda moja baada ya nyingine hadi utafika kileleni.
  Na Malinzi pamoja na kiza totoro alilolikuta wakati anaingia madarakani TFF, aliamua kuanza taratibu ngazi moja, baada ya nyingine na sasa unaweza kusema yuko katikati ya safari.
  Kama binadamu ni mtu anayestahili lawama kidogo, lakini pongezi nyingi kwa makubwa aliyoyafanya Malinzi katika soka yetu ndani ya muda mfupi wa kuwapo kwake, madarakani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAKUNA HAJA YA KUUMIZA KICHWA KUFIKIRIA, NI MALINZI TU! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top