• HABARI MPYA

  Sunday, March 06, 2016

  ACHA YANGA WAICHUKULIE POA APR, INAWEZEKANA WAMEISAHAU, AU HAWAIJUI!

  BAADA ya kuitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 katika Raundi ya Awali ya mchujo Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga sasa itakutana na timu ya Jeshi la Rwanda, APR katikati ya mwezi huu katika Raundi ya Kwanza.
  Yanga iliyoshinda 1-0 Mauritius na 2-0 Dar es Salaam ndani ya wiki mbili, kwa mara nyingine itaanzia ugenini dhidi ya APR, ambayo katika Raundi ya Awali iliitoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 4-1, ikifungwa 1-0 ugenini na kushinda 4-1 Kigali. 
  Mchezo wa kwanza kati ya Yanga na APR unatarajiwa kuchezwa kati ya Machi 11 kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, wakati mchezo wa marudiano utachezwa wiki moja baadaye mjini Dar es Salaam.

  Mapema tu Desemba mwaka jana baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutoa ratiba ya awali ya michuano yake, Watanzania waliipokea kana kwamba Yanga ina mechi mbili nyepesi kabla ya kuanza kukutana na mikiki haswa ya Ligi ya Mabingwa katika Raundi ya Pili, ambako kama itafuzu itakutana na mshindi kati ya Recreativo de Libolo ya Angola na Al Ahly ya Misri.
  Lakini ukweli wa mambo sivyo kama inavyozungumzwa kwamba Yanga imepata mchekea mbele ya APR – kwani timu hiyo ya Jeshi la Rwanda ni imara katika nyanja zote na ina misingi mizuri zaidi kiuwekezaji kisoka kuliko timu ya Jangwani, Dar es Salaam. 
  APR kwa sasa ndiyo inaongoza kutoa wachezaji wengi timu za taifa za Rwanda kuanzia za vijana, timu ya wachezaji wa nyumbani ambayo hivi karibuni ilicheza michuano ya CHAN na kuishia Robo Fainali, ambako ilitolewa na DRC walioibuka mabingwa baadaye.  
  Miongoni mwao, ni beki wa kati, Abdul Rwatubyaye mwenye umri wa miaka 28, ambaye alifunga mabao matatu peke yake (hat trick) katika ushindi wa 4-0 nyumbani dhidi ya Mbabane Swallows mjini Kigali na kiungo Patrick Sibomana aliyefunga lingine.
  Ni APR imara ambayo baada tu ya kufuzu Raundi ya Kwanza, imefanya mabadiliko ya benchi la Ufundi, ikiingia Mkataba na kocha Nizar Khanfir, raia wa Tunisia.
  APR imekuwa chini ya kocha wa akademi yake, Emmanuel Rubona tangu kuondoka kwa Ljupko Petrovic aliyefuatiwa na Msaidizi wake, Mserbia mwenzake, Dusan Dule wakihamia PFC Litex Lovech ya Bulgaria.
  Lakini APR kama Yanga ni miongoni mwa timu bora kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kipindi chote za kuwapo kwao. APR pia imekuwa timu inayoonyesha upinzani mkali kwa Yanga kila zinapokutana.
  Katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika, safari hii inakuwa mara ya pili Yanga kukutana na APR, tena katika hatua hii hii, Raundi ya Kwanza.
  Awali, zilikutana mwaka 1996 na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 3-1, ikishinda 1-0 nyumbani Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 3-0 Kigali.
  APR pia siku zote imekuwa timu yenye kiu ya kufika mbali katika michuano ya Afrika, lakini kikwazo na kukutana na timu ngumu mapema kutoka Kaskazini na Magharibi mwa Afrika.
  Maana yake, bila shaka hata sasa nao wanafurahia kwamba baada ya kutoka Swaziland wanakuja Tanzania, timu ambazo wanaamini zote ni kiwango chao.
  Yanga ni timu ya muda mrefu, lakini kimafanikio katika michuano ya Afrika, wanazidiwa na APR. Mafanikio makubwa ya Yanga katika michuano ya Afrika ni kufika Robo Fainali mara tatu Ligi ya Mabingwa (1969, 1970 na 1998) na mara moja Kombe la Washindi 1995. 
  Lakini APR mwaka 2003 APR ilifika Nusu Fainali ya iliyokuwa ya Kombe la Washindi Afrika, tena ikiitoa US Kenya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa jumla ya mabao 9-2.
  Mechi ya kwanza Aprili 12, mwaka 2003 US Kenya walishinda 2-1, wakati marudiano Aprili 27, mwaka huo, APR  walishinda 8-0 Uwanja wa Amahoro, Kigali.
  Hii inatosha kutoa picha kwamba, APR si timu ya kubeza na inaweza kurudia ilichokifanya miaka 20 iliyopita, iwapo Yanga watashikilia dhana wamepata mchekea na kuacha kuwekeza katika maandalizi mazuri.
  Na kama ambavyo tumeiona Yanga katika mechi za karibuni, ina mapungufu ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi.
  Ina matatizo ya kiuchezaji kwa ujumla, kwani kikubwa wanachojua Yanhga ni kushambulia tu bila kuwa na mipango ya kutengeneza mashambulizi ya uhakika, matokeo yake inaonekana kama wanapoteza nafasi nyingi, kumbe hawana mipango.
  Lakini pia safu ya ulinzi ya Yanga ni jipu ambalo siku likitumbuka pale Jangwani watatafutana. Kwa sasa, Yanga inaweza kufunga timu zenye kufungika tu, lakini ikikutana na timu zilizotulia, watu watashangaa. Wikiendi njema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ACHA YANGA WAICHUKULIE POA APR, INAWEZEKANA WAMEISAHAU, AU HAWAIJUI! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top